Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido Mkoani Arusha Dkt Steven Kiruswa ameahidi kuwasomesha nje ya nchi kwa gharama zake binafsi washindi wa mbio za Kiruswa Fun Run zilizofanyika katika jimbo hilo lengo likiwa ni kuinua vipaji kwa wanamichezo vijana wa mchezo wa riadha katika Jimbo hilo.

Kiruswa alisema hayo mara baada ya kutoa zawadi ya fedha taslimu na vyeti kwa washindi wa mbio za hizo ambazo zilishirikisha mbio za Mita 100,Mita 200,Mita 400,km 5,Km 10 na Km 15 ambapo washiriki mbalimbali katika wilaya ya Longido walishiriki.

Alisema mchezo ni burudani,afya na ajira hivyo yeye kama Mbunge wa Jimbo la Longido ameona jimbo hilo lina vijana wenye vipaji katika mchezo wa riadha hivyo amekiomba Chama cha Riadha Mkoani Arusha{RT} pamoja na viongozi wa Serikali idara ya michezo Longido kuwaandaa washindi wa mbio hizo ili waweze kupata elimu ya michezo katika vyuo vya michezo Nchini jirani ya Kenya kwani nchi hiyo inaongoza kwa kuwa na wanariadha bora Duniani.

Waziri Kiruswa aliwasisitiza viongozi wa RT Mkoa wa Arusha na viongozi wa michezo Longido kuhakikisha kuwa washindi hao wanatunzwa na kupata elimu ya mchezo walioupenda katika vyuo vinavyotambulika Nchini Kenya kwa gharama zake ili kuinua vipaji vya vijana katika Jimbo hilo.

‘’Nimeanzisha ligi ya soka na inafanyika kila mwaka na sasa nimeanzisha mchezo wa riadha ambao kwa utaratibu washiriki hawapaswi kulipwa na sijamtoza mshiriki lakini nimetoa zawadi ya fedha kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu kwa mbio zote lengo ni kutaka vijana wengi kujitoa na kushiriki’’alisema Kiruswa

Naye Mgeni rasmi katika mbio hizo,Afisa Michezo Mkoa wa Arusha,Mwamvita Okeng’o ambaye aliwakilishwa na Afisa michezo wa Arusha,Nestory Dagharo alisema kuwa uamuzi ulianzishwa na Kiruswa unapaswa kupongezwa kwani uamuzi huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi{CCM} katika kukuza michezo nchini.

Okeng’o aliwawataka Wabunge wengine nchini kuiga mfano wa Kiruswa kwani una lengo la kuibua vipaji kwa vijana katika mchezo wa riadha hivyo kampuni na watu binafsi wanapaswa kumuunga mkono Mbunge huyo wa Longido mwenye lengo la kutaka wakimbiaji wapya katika Mkoa wa Arusha.

Naye Afisa michezo wilaya ya Longido,Jesca Rwezaula pamoja na kumshukuru Kiruswa kwa kuanzisha Kiruswafunrun pia alimwomba Mbunge huyo kutatua baadhi ya changamoto katika jimbo hilo ikiwa ni pamoja na wialya hiyo kukosa walimu wa michezo wenye taaluma kwani hiyo ndio changamoto kubwa katika kukuza michezo.

Mmiliki wa mbio za Ruaha Great Marathon,Eward Athanas aliahidi washindi wote wa mbio hizo watakwenda kushiriki mbio hizo Mkoani Iringa kwa gharama zake lengo ni kutaka kuendeleza washindi hao.

Naye Makamu mwenyekiti wa RT Mkoa wa Arusha ,Gerad Babu kwanza alimshukuru,Kiruswa kwa kujitoa na kusaidia kukuza vipaji kwa vijana katika mchezo wa Riadha katika wilaya ya Longido na kusema kuwa chama hicho kitamuunga mkono kwa hali na mali katika kufanikisha malengo yake.



Share To:

Post A Comment: