Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprica Mahundi (Mb) amesema Serikali inatarajia kujenga jumla ya minara 15 katika kata mbalimbali za Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Naibu Waziri Maryprisca amesema hayo tarehe 13 Mei, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Isseke, Wilaya ya Manyoni akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano unaojengwa na kampuni ya simu ya Airtel kwa kushirikiana na UCSAF.

Amesema minara hiyo 15 itajengwa katika kata za Isseke, Makanda, Makutupora, Maweni, Mitundu, Mkwese, Mwamagembe, Nkonko, Rungwa, Sanjaranda, Sanza, Saranda, Sasajila na Sasilo ili kuimarisha huduma za mawasiliano.

Akizungumzia Mnara wa Isseke unaoendelea na ujenzi, Mhandisi Maryprisca amesema umeigharimu Serikali jumla ya Tsh. 116,500,000/- ambapo asilimia 70 ya fedha hizo ambazo ni Tsh. 81,550,000/- tayari zimeshalipwa na UCSAF kwa Airtel.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa mara huo na kuanza kutoa huduma ya Mawasiliano kutawasaidia wakazi wa Vijiji vitakavyofikiwa kwa kuboresha shughuli za kiuchumi na kupata mawasiliano kwa haraka hususan taarifa muhimu za masoko.

Amesema mawasiliano ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Manyoni kwani yatasaidia pia kuokoa muda wa kufunga safari ili kupata huduma umbali mrefu na kurahisisha huduma za kutuma na kupokea pesa ambazo sasa zitatanyika majumbani.

"Tunaishukuru sana kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na UCSAF, kwa kuchukua uamuzi huu wa kuipa Wilaya ya Manyoni kipaumbele na kuamua kufikisha huduma za mawasiliano ya uhakika kwa wakazi zaidi ya 6,900 wa vijiji" Maryprisca.










Share To:

Post A Comment: