Na Fredy Mgunda,Mtama.
TAASISI isiyo ya kiserikali ya Heart to Heart Foundation chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la KOICA imezindua rasmi mradi wa maji na usafi wa mazingira utakaotekelezwa katika Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi.
Akizindua mradi huo utakaotekelezwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart to Heart Foundation chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la KOICA, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Zuwena Omary alisema kuwa ili kufikia mafanikio na malengo ya mradi ni lazima kamati za maji na mazingira zishirikishwe kikamilifu.
Bi Zuwena alisema kuwa suala la upatikanaji wa maji safi na vyoo salama ni lazima kuzingatia utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira ikiwemo upandaji miti na usafi wa mazingira kuzunguka vyanzo hivyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi kutoka Heart to Heart Foundation Ndg. Innocent Deus amesema kuwa mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miaka 3 katika Halmashauri ya Mtama ambapo utazifikia kata 14, vijiji 87, vitongoji 292 na zaidi ya kaya elfu 40.
Innocent alisema kuwa lengo la mradi ni kupeleka huduma ya maji katika vituo vya afya na kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa kuanzia ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya wilaya.
Hivyo, utekelezaji wa mradi huu utaimarisha upatikanaji wa huduma ya afya na kuboresha usafi wa mazingira kwa wananchi. Pia mradi utasaidia kubadili fikra na mitazamo ya wananchi ili waone umuhimu wa matumizi ya vyoo vilivyoboreshwa
Post A Comment: