Na Munir Shemweta

 

Naibu Waiziri Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amewataka watumishi wa Wizara ya Ardhi kutembea kifua mbele na kuacha kuuza utu wao kwa vitu vidogo vidogo.

 

‘’Msiuze utu wenu kwa ajili ya vitu vidogo vidogo nayasema haya mwezi mtukufu, nendeni mkamuombe mwenyezi mungu aendelee kuwasimamia na tuna kila sababu ya kujivunia sisi kupata kazi’’ alisema Mhe, Pinda.

 

Naibu Waziri Pinda amesema hayo tarehe 8 April 2024 wakati wa Iftar iliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya watumishi wake iliyofanyika jijini Dodoma.

 

Amesema, kila wakati anapopata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa wizara yake anajitahidi kuwakumbusha maeneo ambayo yanaifanya wizara ya ardhi kuwa na malengo.

 

Amewahimiza watumishi wa sekta ya ardhi kutotoa huduma kwa kuangalia hali za watu na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia haki na kusisitiza kuwa, kwa waislamu waliofunga funga yao itapokelewa kwa mwenyezi mungu.

 

Mhe, Pinda amewakumbusha watumishi hao kufanya kazi kwa utiifu wa maelekezo ya Mwenyezi Mungu aliyoyaeleza kuwa yanatokana na vitabu vyake vitakatifu na kwa hakika watabalikiwa.

 

Aidha amewafikishia salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia kwa kupongeza mabadiliko makubwa ya kiutendaji ya Wizara ambapo amewataka watumishi hao kutobweteka ili kuyaishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassani.  

 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Bi. Lucy Kabyemera amesema tukio la kuandaa futari kwa ajili ya mwezi mtukufu wa ramadhani siyo dogo kwani linaleta umoja na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Wizara ya ardhi.

 

Ameweka wazi kuwa, watumishi wanafarijika sana wanapoona viongozi wakuu wa Wizara wanafika kwenye matukio muhimu kama vile tukio la iftar pamoja na yale ya huzuni jambo alilolieleza linajenga umoja na kutia moyo kiutendaji.

 

‘’Umekuwa ni utaratibu wa mara kwa mara kwa Wizara kuandaa futari kwa watumishi kwa lengo la kujenga uhusiano na mshikamano kwa katika Wizara yake’’. Alisema Lucy

 

Ametaka tukio la iftar lililoandaliwa na wizara yake liwakumbushe watumishi wa wizara hiyo kushikamana, kufanya kazi kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa weledi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza majukumu hususan ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya ardhi.

Share To:

Post A Comment: