Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inarejesha miundombinu ya barabara ya Kasansa - Muze - Mtowisa - Ilemba - Kaoze - Kilyamatundu (km 180) iliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo tofauti tofauti nchini.

Bashungwa ameeleza hayo Aprili 08, 2024 Mkoani Rukwa wakati akikagua barabara hiyo na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya  matengenezo makubwa katika maeneo korofi ya Nkwilo, Mtowisa, Zimba,  Kisa, Kinambo, Ilemba na Solola ambayo yameathiriwa kwa kiasi kikubwa.

“Niwaahidi wana Rukwa, Serikali itaendelea kufanya kila jitihada kurejesha miundombinu katika maeneo yaliyoharibiwa na mvua kadri inavyowezekana ili huduma za kijamii na kiuchumi ziweze kuendelea kama kawaida”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema Wizara  ya Ujenzi italeta wataalam wa miamba kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina katika Milima ya Ufipa hasa katika eneo la Nkwilo ambapo kuna changamoto ya mawe mengi yaliyoshuka kutoka Milimani ili tathimini hiyo ilete suluhisho la kudumu katika miundombinu iliyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa.

Kutokana na ombi la Mbunge wa Jimbo la Kwera, Deus Sangu la hitaji la kuunganisbwa kwa barabara ya eneo la Muze kuelekea Sumbawanga na barabara ya Ilemba kuuganishwa na Mkoa wa Songwe, Waziri Bashungwa amesema Serikali inepokea ombi hilo ili kulifanyia kazi.

Bashungwa amempongeza Mkurugezi wa Matengenezo kutoka TANROADS, Dkt. Christina Kayoza pamoja na Mameneja wa Mikoa wa TANROADS kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanarejesha miundombinu ya barabara kwa haraka pindi inapoharibiwa na mvua.

Vilevile, Bashungwa ametoa wito kwa wananchi na waendesha vyombo vya moto kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua za El-Nino, pale wanapokuta barabara au madaraja yamejaa maji waweze kusimama na kuyasubilia yapungue ndipo wapite.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Eng. Mgeni Mwanga ameeleza kuwa barabara zilizoathiriwa zaidi na mvua ni barabara ya Kasansa - Muze, Muze - Mtowisa, Mtowisa - Ilemba na Ilemba - Kaoze, ambapo TANROADS imerejesha mawasilino ya barabara wakati wakisubiria kufanya matengenezo makubwa.

Naye , Diwani wa Kata ya Zimba, Efraim Konta, ameishukuru Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi kwa kuweza kufika Wilayani Sumbawanga kurejesha mawasilino hayo ya  barabara hiyo ambayo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi kusafirisha mazao kutoka Mkoani Rukwa kwenda Mkoa wa Songwe na mikoa jirani.


Share To:

Post A Comment: