Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda kilichopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi wametakiwa kusoma kwa bidii na malengo ili wapate kile walichokusudia kukipata kwenye chuo hicho.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 15 April 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe. Geophrey Pinda alipokutana na kufanya mazungumzo na wanafunzi wa chuo hicho cha Kilimo kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.

 

Amesema, ni vyema wanafunzi wanaosoma chuo hicho Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi kuangalia malengo yaliyowapeleka chuoni hapo sambamba na yale ya wazazi wao ili kupata kile wanachohitaji kutoka chuo hapo.

 

"Kama umekubali kuja katika chuo cha Katavi ambacho kiko mbali na macho yaliyo wazi na umekubali kuja hapa kuwa ‘serious’ na masomo yako utapata kitu kikubwa sana" alisema Mhe. Pinda.

 

Wanafunzi wa chuo hicho ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro mbali na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Kavuu mkoani Katavi kwa kuwatembelea ili kujua changamoto zinazowakabili, wamemuomba kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali chuoni hapo ikiwemo kupatiwa Mizinga ya Nyuki kwa ajili ya Masomo ya Vitendo, Mipira kwa ajili ya mpira wa Miguu na Pete pamoja na Televisheni.

 

Aidha, wamemuomba kusaidia upatikanaji mikopo kwa wale wanafunzi wasiopata mikopo ya elimu ya juu. Wamesema pamoja na mikopo kupatikana kwa asilimia tofauti kwa wanafunzi wa chuo hicho lakini wapo baadhi yao hawakupata kabisa jambo linalowafanya kuishi kwa shida.

 

"Ukiangalia mtu hana uwezo na mfano ni kwa mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo chetu wakati mwingine inatulazimu sisi wanafunzi wenzake timchangie" Wamesema wanafunzi.

 

"Hapa kuna wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawajapata mikopo ya elimu ya juu na yupo mmoja ukimuangalia hana uwezo kabisa tulilazimika kumchangia fedha". Walisema.

 

Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi Prof Anna Sikila amesema, pamoja na chuo hicho kuwa na mazingira mazuri lakini wanafunzi wamekuwa wakisoma vizuri na kujituma katika masomo yao.

 

Kwa mujibu wa Profesa Sikila, kujituma na kusoma kwa bidii kwa wanafunzi wa chuo hicho kumesababisha mwaka jana 2023 mwanafunzi kutoka chuo hicho kuongoza kimasoma kwa vyuo vyote viwili vya Morogoro na Katavi.

 

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda kinatoa kozi tatu za Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki, Stashahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao pamoja na Astashahada ya Uongozaji Watalii na Uwindaji wa Kitalii.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati wa kikao chake na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokione cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi. Kulia ni Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Profesa Anna Sikila na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano Debora Magesa.
Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila akizungumza wakati wa kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (Kushoto) na wanafunzi wa chuo hicho tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa katavi. Kulia ni Rais wa Serikali ya wanafunzi William Bulongo.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Geophrey Pinda (Hayupo pichani) wakati wa kikao chao kilichofanyika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024.

 
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Geophrey Pinda (Hayupo pichani) wakati wa kikao chao kilichofanyika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa tatu kulia), Naibu RASI wa Ndaki  Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Anna Sikila (wa kwanza kulia), Rais wa Serikali ya Wanafunzi William Bulongo pamoja na Wakuu wa idara wa chuo hicho wakiondoka mara baada ya kikao chao kilichofanyika chuoni hapo tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia) akizungumza na Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila (kulia) mara baada ya kikao chake na wanafunzi kilichofanyika chuoni hapo katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024. Wengine pichani ni wakuu wa Idara za ICT na Usimamizi Rasilimali Nyuki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa tatu kulia) pamoja na RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa chuo hicho mara baada ya kuzungumza nao tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
Share To:

Post A Comment: