Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro akitoa ufafanuzi na maelekezo katika kero na malalamiko yaliyozungumzwa na wakazi wa tarafa ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga

TAZAMA VIDEO YOTE WANANCHI WAKILALAMIKA DC MTATIRO AKIJIBU

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwenda kuweka kambi maalum kwa ajili ya kushughulikia kero za wananchi wanaodai kukosa haki zao katika tathimini iliyofanyika kwenye makazi ya maeneo yao katika uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Shinyanga uliopo kata ya Ibadakuli.

DC Mtatiro ametoa maagizo hayo  Aprili 5,2024 kwenye mkutano wake wa hadhara, baada ya kusikiliza na kupokea kero na malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wananchi wakazi wa tarafa ya Ibadakuli.

 Baadhi ya wananchi hao wamelalamika kukosa haki yao stahiki katika maeneo waliyokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao za kila siku ambapo kwa sasa eneo hilo limechukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Shinyanga.

Wamesema fedha ya fidia inayotolewa na serikali haiendani na ukumbwa wa maeneo yao ambapo wamesema tathimini iliyofanyika katika maeneo yao haikuzingatia utaratibu ulioweka na serikali.

Mmoja wa wananchi aliyelalamika katika mkutano huo wa hadhara ni Joyce Bala Lukale ambaye amesema amepewa fidia ya fedha shilingi laki nne kwenye eneo lake ya hekari saba.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuitaka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwenda kushughulikia changamoto ya malalamiko ya wananchi hao ili waweze kupata haki zao stahiki.

“Suala la fidia na tathimini nadhani kwamba linashida tathimini inapofanywa  mahali inakamilika Halmashauri ya Manispaa zinahusika moja kwa moja asilimia mia moja kwa nini zinahusishwa Halmashauri kwa sababu ni serikali za mitaa ninachotaka kuzungumza ni kwamba sisi kwa upande wa serikali tujipange wanaishi wanaeleza unajua kabisa hajatendewa haki, mtu anahekari aba za maeneo ana mazao kwenye maeneo ana miti halafu eti anakuja anapewa fidia ya laki nne siyo tathimini hiyo hii ni felia na watumishi wa serikali tusikubali hii felia maana tathimini ni haki ya mtu”.

“Kwahiyo mimi nasema pamoja na kwamba tunaendelea kupambana kutatua hizo changamoto lakini Halmashauri mjue mimi pale ambapo naongoza kama mkuu wa Wilaya sihitaji kuondoka na laana za wananchi kwamba nilishiriki kwenye tathimini na wananchi wakaibiwa hela zao kwa sababu haya ambayo yamefanyika siyo mfano mzuri”.

“Mhe. Rais ataka haki hii michezo ifike mwisho na mimi nitawaandikia barua maalum TANROADS, mthamini mkuu wa serikali pamoja na Manispaa hii, hili haliwezekani wananchi wanathaminishiwa haki yao inakuwa A halafu anakuja kulipwa B kwahiyo Manispaa nawaagiza kuja kuweka kambi hapa mrudi hapa mpige kambi na nawapatia Mwezi huu wa nne narudia tena mrudi hapa mpige kambi kwahiyo nikirudi hapa kwenye mkutano wangu mwananchi akisimama kuzungumzia tathimini kuwa na majibu”.amesema DC Mtatiro

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro pia amesema haridhishwi na utendaji wa wakala wa barabara za vijijini na mijini TARURA Wilaya ya Shinyanga katika utekelezaji wa miradi yao.

“Kati ya eneo ambalo siridhishi toka nimekuja hapa kama mkuu wa Wilaya, siridhishi na utendaji wa TARURA kuna maeneo mengi nakwenda kuna miradi mingi nimekwenda ambayo wakandarasi wanapaswa kuwa site lakini hawako site na siyo tarafa hii peke yake tarafa zote nilizopita nadhani kuna shida kwahiyo mimi nasema hii kasi ya utendaji wa TARURA Shinyanga siridhishwi nayo na wakiendeleea namna hii tutamtaarifu mkurugenzi mkuu maana hawa wakandarasi waliopewa  fedha ambazo ni fedha za walipa kodi fedha za nchi yetu watekeleza matengenezo ya barabara mbalimbali za Shinyanga wanapaswa kuwa site Shinyanga ni Manispaa hauwezi kuja hapa tu Ibadakuli vijiji havina barabara kuna shida gani”.amesema DC Mtatiro

Aidha DC huyo Wakili Julius Mtatiro amesikiliza na kupokea kero mbalimbali kutoka wa wakazi wa tarafa ya Ibadakuli  ambapo amewahakikishia wananachi hao kuwa kamati yake ya kuchunguza na kushughulikia malalamiko itafika katika maene yao kufahamu zaidi kero zao ili serikali iweze kuchukua hatua haraka.

Pia katika ziara zake DC Mtatiro ametembelea tarafa mbalimbali sita za Wilaya ya Shinyanga ikiwemo tarafa ya Old Shinyanga pamoja na tarafa ya mjini ambapo amehitimisha ziara yake katika tarafa ya Ibadakuli na kwamba ameahidi kuwa kamati aliyoiunda itatekeleza majukumu yake kwa weledi ili kila mmoja aweze kupa haki yake.

Kupitia mkutano huo baadhi ya wananchi waliozungumza na Misalaba Media wamempongeza mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro kwa kutoa nafasi ya kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi,hali wanayoitaja kuwa ni uongozi uliotukuka.

Share To:

Misalaba

Post A Comment: