Wananchi hao wamesema wanalazimika kunywa maji hayo kutokana na mgao mkubwa wa maji uliopo katika kitongoji hicho kwa mwezi wanapata mgao wa maji mara moja au kukosa kabisa.

wananchi hao waliendelea kusema licha ya kila mwananchi kuunganishiwa maji kwa gharama ya Sh162,000 mwaka 2018 changamoto ya maji imeendelea kuwepo katika kitongoji hicho hali ambayo imekuwa ikisababisha kero kwa wananchi.

Yasinta Mushi, mkazi wa kitongoji cha Singa kati, wilayani hapa, amewatupia lawama viongozi wanaosimamia miradi ya maji katika kijiji hicho na kusema kwamba changamoto hiyo ya maji inasababishwa na wao baada ya kutokusimamia miradi ya maji katika kijiji hicho.

“Tuna changamoto kubwa sana ya maji hapa, changamoto hii inatokana na viongozi waliopo ambao wanasimamia miradi hii ya maji, haya maji sisi wenyewe ndio tumechimba miaka hiyo na baadaye tuliambiwa ukitaka kufungiwa maji unalipa Sh 162,000 tulifanya hivyo, lakini mpaka leo hatuji hizo fedha zilienda wapi,”

“Nimefunga bomba nyumbani kwangu na nilitoa Sh162,000 cha kushangaza mpaka sasa sina maji, maji hayatoki bombani, tunaomba serikali ituangalie maana maji tumechimba wenywe na tumechangia fedha, na hatujui ziko wapi na sisi tunaendelea kuteseka kwa kukosa maji,”

Aliendelea kusema “Tunazungumza hivi, mpaka sasa sina maji nyumbani kwangu, tunalazimika kutumia maji machafu maana hatuna maji, inabidi uende mtoni au kwenye mfereji kuchota maji ya matumizi ya nyumbani, tunaomba serikali itupe msaada ili haya maji yetu tuliyopambana nayo wenyewe tuweze kunufaika nayo,”

Mariham mbaruk, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, amesema wakati mwingine wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kusaka maji ya mto karanga kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani ikiwemo kupikia na kunywa kutokana na changamoto ya mgao wa maji.

“Mgao wa maji umekuwa ni changamoto kubwa, hapa kwetu zinapita siku kumi na zaidi huoni maji kwenye bomba, zaidi wakati tulipofungiwa haya maji tulihakikishiwa uhakika wa maji, chakushangaza imekuwa ni kinyume chake, tunataabika sana tunaomba serikali kupitia wizara husika ije ione changamoto hii ya maji tunayopiti,”

 

Naye, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Aloyce Chuwa, alisema awali wananchi wa kijiji hicho walikuwa na mradi wao wenyewe wa maji na kwamba baadaye maji yale yalitawanywa maeneo ya vijiji vingine, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa wananchi hao kukosa maji.

“Changamoto tuliyonayo hapa kijijini kwetu ni suala la maji, tuna maji ya bomba lakini maji haya mara kwa mara hatuyapati, tulichangia nguvu kazi yetu kuvuta maji na baada ya kupata maji kutoka huko msituni tukawa na mradi wa kijiji, baadaye tuliambiwa sio mradi wa kijiji tena na kwamba tumeunganishwa na kata za jirani,”

Amesema wananchi wanaweza kukaa kwa siku sita mfululizo au zaidi bila maji na kwamba tatizo la maji limeendelea kuwaumiza wananchi kwani baadhi yao wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji mtoni maji ambayo sio safi na salama.

“Watu wakikosa maji kwenye bomba, wanaenda kuchota maji mtoni ya kunywa pamoja na matumizi mengine ya nyumbani, na haya yanaweza kutuathiri kiafya kwa kuwepo na magonjwa ya tumbo , maana kipindi cha nyuma watu walihara kwa kunywa maji ya mtoni,”amesema mwenyekiti huyo

Joseph Ngowi, Mwenyekiti wa kitongoji cha Singa Kifueni, alisema baada ya mradi wa maji kusimamiwa na taasisi ya SIKIKA ufanisi wake umekuwa mdogo na kusababisha wananchi kukosa maji kila mara hali ambayo inaleta usumbufu kwa wananchi.

“Mwaka tuliletewa watu wanaoitwa SIKIKA kuchukua nafasi ya jumuiya watumia maji iliyokuwa hapa kijijini, mpaka sasa wananchi bado hawajaelewa hii taasisi inafanya kazi gani hapa, tumefanya vikao bila mafanikio, changamoto imeendelea kuwepo ya maji, wananchi wanaendelea kutaabika bomba hazitoi maji,”

Aliongeza “Mwanzoni kabisa, tulichangia nguvu kazi kwenda kuchimba maji kutoka msituni kuja kwenye maeneo ya wananchi, tulitoa nguvu kazi asilimia 25 na hiyo nyingine tulisaidiwa na Wajerumani waliokuwepo hapa kijijini tukapata maji ya uhakika sasa ilipokuja hii taasisi imelkuwa ni changamoto sana,”

 

Alipotafutwa Meneja anayesimamia mradi wa maji kijijini hapo, kutoka taasisi ya SIKIKA, Mwita Juma alikiri uwepo wa changamoto wa maji katika baadhi ya maeneo katika kijiji hicho, na kwamba jitihada zinafanyika kuhakikisha wananchi wanapata maji.

“Mafundi ambao wanahudumia mradi huu wapo watatu kuna eneo letu moja lipo Uchao kusini na Maua ndio kuna changamoto ya maji, sasahivi tunaongeza nguvu katika maeneo hayo na baada ya kumaliza watahamia eno la Singa ambalo lina changamoto ya maji, hivyo uvumilivu unahitajika”

Share To:

Post A Comment: