Katika hatua ya kuimarisha Huduma za Afya na kutoa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa ya mlipuko, Wizara ya Afya na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametoa Televisheni 57 kwa vituo vya kutolea huduma za Afya 57 katika mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Kagera, na Singida.

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa, amekabidhi Televisheni hizo leo, Februari 07, 2024, amesema kuwa la ugawaji wa televisheni hizo ni katika kuendelea kutoa elimu kuhusu njia za kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.

 

Dkt. Rutachunzibwa amesisitiza umuhimu wa Televisheni hizi katika kuelimisha jamii kuhusu mbinu za kuzuia na kudhibiti maambukizi ya magonjwa ya mlipuko, akiongeza kuwa ni sehemu muhimu ya mkakati wa kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii.

 

Kwa upande, Afisa Uhusiano kutoka REA Jaina Msuya amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu na kuwanufaisha wengi zaidi.

 

Aidha Mwakilishii kutoka Wizara ya Afya, James Mhilu ameeleza dhamira ya wizara katika kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia mradi huo wa kusambaza Televisheni na kwamba Televisheni hizo zitasaidia sana katika kutoa elimu ya afya kwa jamii, hususan katika maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za afya na habari ni changamoto.

 

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Flora Freddie, ameahidi kwamba vifaa hivyo vitatumika kama ilivyokusudiwa, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

 

Hatua hii inaonesha ushirikiano kati ya serikali na mashirika mbalimbali katika kuboresha huduma za afya na kutoa elimu muhimu kwa jamii.

 

Share To:

Post A Comment: