Watumishi na watoa huduma za afya wamesisitizwa kuzingatia weledi na miiko ya taaluma zao wanapotekeleza majukumu yao ili kuipa thamani Miradi na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya Afya Nchini.

Msisitizo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya *Dkt. Grace Magembe Februari 20, 2024* wakati wa ukaguzi wa Miradi ya ujenzi na usimikaji vifaa tiba inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Sekou Toure, Hospitali ya Halmashauri ya Jiji la Nyamagana na Hospitali ya Kanda Bugando zote za Mkoani Mwanza. Amesema Serikali inatoa fedha nyingi katika kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya nchini lakini kumekuwapo na baadhi ya watoa huduma ambao sio waadilifu na kufanya jitihada hizo zisionekane.

“Ndugu zangu huu uwekezaji ni mkubwa sana kutokea katika miaka 3 iliyopita. Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya jukumu lake, kazi iliyobakia ni sisi kutekeleza wajibu wetu na hasa watoa huduma za Afya, tubadilike tuache kufanya kazi kwa mazoea, kila taaluma katika sekta ya afya inayo miiko yake lazima kila mtu afanye kazi kwa kuzingatia miiko na weledi wa taaluma yake” amesema Dkt. Magembe.

“Hakutakuwa na kupepesa macho, tutachukuliana hatua, tutatoa nafasi ya kufundishana, kuelekezana na kurekebishana, yote hayo yakishindikana tutachukua hatua kali zaidi. Tumeshuhudia baadhi ya wenzetu ambao wamefutiwa usajili na mabaraza yao ya taaluma, wamesimamishwa kazi kwa miaka kadhaa, wengine wamerudishwa vyuoni” na wengine kufukuzwa kazi kabisa amesema Dkt. Magembe.

Aidha Dkt. Magembe amesema Serikali itawapa motisha mbalimbali watoa huduma ambao watafanya vizuri ikiwa ni sehemu ya kutambua utendaji wao mzuri wa kazi.

Naibu Katibu Mkuu yuko ziarani kanda ya Ziwa kukagua utekelezaji wa miradi ya Afya na utoaji wa huduma.Share To:

Post A Comment: