Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastun Kitandula (Mb) amewataka Makamishna wa Uhifadhi wa Taasisi zote za Jeshi la Uhifadhi nchini kuhakikisha Askari wanaohitimu mafunzo watumike ipasavyo katika kuchochea kasi ya mapambano dhidi ya ujangili wa Wanyamapori na rasilimali za Misitu.
Mhe. Kitandula ametoa rai hiyo leo Machi 23, 2024 wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa Askari 296 wa jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu katika Kituo cha mafunzo cha Mlele, Mkoani Katavi
“Natumia fursa hii kuwapongeza wahitimu wote 296 kwa kuhitimu mafunzo haya muhimu ya awali ya kijeshi na pia, napongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Wizara kupitia kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, wakufunzi wa mafunzo haya kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na wakufunzi wa ndani kutoka Jeshi la Uhifadhi,” Mhe. Kitandula amesema
Aidha, amewataka Askari hao kutanguliza mbele uzalendo na uadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwataka kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Natambua kwamba kumekuwepo na baadhi ya Askari wasio waadilifu wanaokiuka maadili na miiko ya kazi zao kwa kujihusisha na upokeaji wa rushwa pamoja na kutumia nguvu kupita kiasi, hili halikubaliki hata kidogo" amesema Mhe.Kitandula.
Kufuatia vitendo hivyo, Mhe.Kitandula ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa askari huku akitoa msimamo wa Serikali kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha vitendo hivyo kwa namna moja ama nyingine atachukuliwa hatua kali za kisheria
“Ni matarajio yangu mtatekeleza kwa vitendo na kwa weledi mkubwa yote mliyojifunza katika muda wote wa utumishi wenu katika Taasisi zenu chini ya mwamvuli wa Jeshi la Uhifadhi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata taratibu na miongozo yote ya Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu,” ameongeza.
Baadhi ya mambo muhimu ambayo Askari hao wamejifunza wakati wa mafunzo yao ni pamoja na mbinu za medani, utawala na uongozi, uzalendo, jinsi bora ya kufanya doria, amri za jumla (General Order), matumizi ya silaha mbalimbali za kivita, kwata mbalimbali, Maadili ya viongozi na wafuasi wao, heshima na nidhamu ya kijeshi, falsafa ya salamu ya kijeshi, utoaji wa huduma ya kwanza, ukamataji salama, taratibu za upekuzi na uchunguzi, kukabiliana na majanga ya mioto katika misitu na wanyamapori, usomaji ramani na mengineyo muhimu.
Nafahamu kuwa mafunzo haya hayakuwa mepesi, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wenu ni mara ya kwanza kupata mafunzo ya namna hii, pia natambua kuwa katika kipindi chote cha mafunzo mmejifunza mambo mengi kwa nadharia na vitendo,” Naibu Waziri Kitandula amewaasa wahitimu.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri Kitandula amezitaka Taasisi zinazounda Jeshi la Uhifadhi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa awali kwa kutenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya kukarabati na kuboresha miundombinu iliyopo pamoja na kujenga miundombinu mingine mipya ili iendane na mahitaji ya kituo na mafunzo yanayotolewa.
“Ni matumaini yangu kwamba katika mwaka wa fedha ujao (2024/25) kituo hiki kitajengewa mazingira bora ya miundombinu kulingana na mahitaji ya sasa katika kuimarisha Uhifadhi wa rasilimali za Wanyamapori na Misitu hapa nchini,” alisisitiza.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dustan Kitandula (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, CP. Benedict Wakulyamba amewaasa Askari hao kuwa makini katika utekelezaji wa majuku yao huku akisisitiza kuwa jukumu la askari hao ni kutoa huduma ya kulinda Rasilimali za nchi hii hivyo waitende kazi hiyo kwa ueledi mkubwa.
Ameongeza ya kuwa jukumu la Jeshi la uhifadhi ni kuwa nidhamu, uaminifu na uadilifu, huku akiwataka Askari hao kuyafuata hayo ili kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yao
“Jeshi ambalo halina nidhamu, uadilifu na uaminifu ujue ni jeshi la majangiri ambao wamevaa uniform, Tusingependa muwe hivyo niwaombe sana mzingatie haya’’ Alisema CP Wakulyamba
Post A Comment: