Na Joel Maduka ,Kahama


Serikali imesaini Mkataba wa ujenzi wa  Barabara ya urefu wa Kilomita  73 kwa kiwango cha lami   inayotoka  Bulyanhuru Kijiji cha Kakola Kuelekea Kahama Mjini ,huku malengo yake makubwa ikiwa ni kufungua fursa za kiuchumi  upande wa madini ,Kilimo ,Misitu na utalii kwenye mikoa ya Shinyanga ,Geita,Kagera,Tabora na Kigoma.

Mkataba huo umesainiwa kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya Shilingi Bilioni 101.2 kwa ufadhili wa Kampuni ya Madiniya Barrick Tanzania Mining Companies (BTMCs) na Serikali ya Tanzania.

Akishuhudia Utiaji Saini wa barabara hiyo  kwenye Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Mbunge Msalala Iddi Kassim Iddi amesema pamoja na utiaji saini wa barabara hiyo bado serikali imesaidia kutoa kiasi cha milioni  mia tano kwaajili ya kuweka lami ya km 1 kwenye eneo la Kakola,Bulige,Segese na Ngaya ambapo hadi sasa mkandarasi tayari yupo eneo la shughuli.

“Mhe waziri ni ukweli nimekuwa nikikusumbua juu ya ujenzi wa Barabara ya Kakola kuja Kahama maana tulikuwa tukitengeneza baada ya siku tatu inaharibika matusi kwenye mitandao yalikuwa ni mengi lakini leo tunakwenda kufungua rasmi ujenzi wa barabara hii ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni kilio chetu wanamsalala”Iddi Kassim Iddi Mbunge Jimbo la Msalala.

“Ni ukweli nikili ujenzi wa Barabara hii umechelewa na wengi wananchi wamekuwa na maswali ni kwanini Barabara imechelewa nataka niseme tu jambo  moja  Barabara ambayo leo inatiwa saini ilitakiwa ijengwe Bulyahulu kwenda Mwanza ,na fedha zilikuwa tayari zimeshatengwa lakini mimi nilimfuata Waziri wa Madini wa kipindi hicho Dkt Biteko na kumuomba  wabadilishe uelekeo kwani barabara yenye masirahi na wananchi ilikuwa ni ya Kakola Kahama”Iddi Kassim Iddi,Mbunge Msalala.

“Niseme Kutoka Moyoni Tunamshukuru Sana Mhe,Rais Dkt Samia Kwani yeye ndiye chanzo cha leo tunashuhudia mkataba ukiwekewa saini na mkandarasi pamoja na TANROAD Rais ametusaidia sana tunamuhaidi  kutokumuangusha 2025”Iddi Kassim Iddi Mbunge Jimbo la Msalala.

Naye Waziri Ujenzi ,Innocent Bashungwa ameeleza kuwa barabara hii imekuwa ni kilio cha muda mrefu na sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri na wawekezaji wa ndani ya nchi ikiwemo kampuni ya Barick ametoa kibali barabara hiyo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mhe. Rais pia ameelekeza Wizara ya Ujenzi kuanza hatua za kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Iloginhadi Mtakuja (km 57.4)  ambayo ni barabara ya kiuchumi na inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Geita.

Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa mtandao wa barabara kwa zile za changarawe na zile za lami zilizopo Mkoani Shinyanga zitaendelea  kusimamiwa na kuhudumiwa ili ziweze kupitika msimu wa kiangazi na vuli ikiwemo barabara ya Old Shinyanga - Solwa - Burige mpaka Kahama pamoja na ile Kolandoto-Lalago.

Bashungwa amemtaka Mkandarasi huyo kuona namna ya kuchangia huduma za kijamii kwa wananchi wanaouzunguka mradi huo pamoja na kushirikiana na wananchi wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Mohamed Besta ameeleza kuwa Mkandarasi aliyeshinda zabuni ni Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa muda wa Miezi 27 na kusimamiwa na TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU).

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala Mlolwa, ameomba ujenzi wa barabara uanzie katika mji wa Kakola ambapo wananchi wengi wamekiwa wakiteseka kwa ubovu wa barabara na kusisitiza mradi huo uweze kukamilishwa kabla ya muda uliopo kwenye mkataba kwa kuwa ana imani na kasi ya Serikali katika utekelezaji wa miradi.

Share To:

Post A Comment: