Ashrack Miraji, (Same) Kilimanjaro. 


Wanakijiji wa  Singa,kata ya Kibosho Mashariki mkoani Kilimanjaro wameonesha kufurahishwa kwa kujengewa zahanati na Mdau wa maendeleo Joseph Mushi ambaye amechukua hatua ya kujenga zahanati ya kisasa kwa ajili ya jamii yake iliyokuwa awali ikiteseka kwa kukosa huduma za afya.


Zahanati hii itakuwa na huduma bora za afya na itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi  zaidi ya  4000 wa kijiji hicho.Kwa muda mrefu, wananchi wa kijiji hiki wamekabiliwa na tatizo la kukosa huduma za afya karibu na makazi yao.


Akizungumza na Vyombo vya habari,Mdau wa maendeleo nchini, Joseph Mushi amesema zahanati hiyo itakuwa chachu ya Maendeleo kijijini hapo kutokana na kwamba awali wakazi hao waliishi maisha ya wasiwasi  kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya hasa nyakati za usiku.



"Kwa mapenzi yangu ya dhati nimeamua kujenga zahanati iwasidie wananchi kijiji hiki na vijiji  jirani vinavyoizunguka zahanati hii,tayari imekamilika asilimia zote tunatarajia kuifungua mwishoni mwa mwezi huu baada ya kukamilisha taratibu za kiserikali kupata vibali "amesema  Mushi.


Ameongeza kuwa kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo, wanakijiji hao walienda kutibiwa Kibosho Hospital umbali wa zaidi ya kilomita tano lakini sasa wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu  kufuata huduma za afya.


Wakati huohuo  baadhi ya wananchi waliofika kutembelea zahanati hiyo wamemshukuru Mdau wa Maendeleo huyo kwambai zahanati iliyojengwa itaepusha vifo vilivyotokana na kuchelewa kupata huduma za afya.



"Kwa kweli zahanati hii itatusaidia sana,hivyo jukumu letu ni kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kizazi na kizazi kikute huduma hizi zikiendelea,”amesema  David Masawe Mkazi wa Kijij hicho.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji Cha Singa,Aloyce Chuwa amesema mdau huyo amekuwa msaada kwa wananchi kwamba awali wajawazito walipata shida ya kupata huduma, hali ambayo ilisababisha wengi wao kujifungulia njiani na wengine kupoteza watoto.


"Kutokana na huduma hii ambayo ameitoa katika kijiji chetu hatuna budi kumuunga mkono kwenye masuala ya Maendeleo katika kijiji hiki maana amekuwa mtu wa watu niseme tu  hii zahanati itakwenda kuwasaidia na vijiji vya jirani si tu kijiji cha  Singa pekee"  amesema Chuwa







 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: