Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akiongea katika hafla hiyo.
Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Abdala Mwaipaya, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,akizungumza katika hafla hiyo.
Mwanzilishi wa Maktaba jamii ya Martha Onesmo, Jennifer Dickson, (kushoto mwenye Tshirt nyeupe) akitoa maelezo jinsi maktaba hiyo itakavyohudumia wananchi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (katikati) na viongozi wengine wa Serikali na Dini wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika viwanja vya usharika wa Kisangeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mwanzilishi wa Maktaba jamii ya Martha Onesmo, Jennifer Dickson, (kulia mwenye Tshirt nyeupe), akitoa maelezo jinsi maktaba hiyo itakavyohudumia wananchi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, (wa pili kutoka kulia) wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika viwanja vya usharika wa Kisangeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.wengine pichani ni Askofu wa Dayosisi ya Mwanga Chediel Sendoro na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo (kushoto).
Baadhi ya wageni waliohudhuria katika hafla hiyo wakifuatilia matukio .
Na Mwandishi Wetu
MAKTABA mpya ya kijamii inayojulikana kwa jina la Martha Onesmo, iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa wilaya ya Mwanga, imezinduliwa katika kata ya Msangeni, ambapo hafla ya uzinduzi ilifanyika katika katika viwanja vya kanisa la KKKT usharika wa Kisangeni na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali na wananchi wa eneo hilo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda. Maktaba hiyo imeanzishwa na kijana wa kitanzania anayesoma Chuo Kikuu nchini Rwanda, Jennifer Dickson.
Akiongea katika hafla hiyo,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, alimpongeza mwanzilishi wa mradi huo Bi. Jennifer Dickson, ambapo alisema maono yake, (ya Jennifer) yatachangia maendeleo ya watu wengi watakaotumia maktaba hiyo.
“Maktaba hii imekuja wakati muafaka ambapo Serikali imekuja na mabadiliko ya mfumo wa elimu yenye lengo la kuboresha elimu ya Watanzania kwa kuwa maktaba itatumiwa na wanafunzi, walimu na wakazi wengine kujiongezea maarifa”. alisema.
Aliongeza, “Jennifer maono yako yametupa matumaini kwa serikali kuwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu ni salama kwa sababu ina vijana wabunifu kama wewe; nikuhakikishie wewe na waliohudhuria hafla hii kuwa serikali itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha maktaba hii inakuwa endelevu”.
Alisema Serikali imeanza kutekeleza mpango unaolenga kuboresha maktaba zote nchini ili kutoa fursa kwa wanafunzi, walimu na wakazi wengine wa ndani na wanaoishi nje ya nchi kupata ujuzi wa ziada na tayari imetenga takribani shilingi bilioni 2 kutekeleza suala hilo sambamba na kuboresha maktaba 22 katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maarifa zaidi kupitia maktaba hizo.
Naye Mwanzilishi wa maktaba hiyo, Bi. Jennifer Dickson, alisema ameanzisha maktaba hiyo ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu aliyokuwa nayo kwa miaka mingi ya kuhakikisha wakazi wa vijijini wanafikiwa huduma za maktaba ili waweze kupata maarifa.
“Maktaba hii inayoitwa Martha Onesmo, ni kwa ajili ya kumuenzi bibi yangu, ni ndoto niliyoota tangu nasoma kidato cha sita, ninafuraha kuwa ndoto hiyo imetimia. Maktaba hii pia ni mchango wangu na wale walioniunga mkono, katika kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuboresha sekta ya elimu nchini”.alisisitiza.
Bi Jennifer, aliendelea kusema kuwa maktaba hiyo ambayo alisema pia ina baadhi ya michango kutoka kwa wanajumuiya wa Msangeni itakuwa kituo cha mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya aina nyingine kwa ujumla itakayochangia maendeleo ya taifa na kutoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kutumia huduma za maktaba kujisomea ili waweze kupata maarifa na kuachana na dhana potofu kuwa maktaba ni za wanafunzi, walimu na wasomi pekee.
Alitoa shukrani kwa wafadhili mbalimbali waliomwezesha kutimiza ndoto yake baadhi yake akiwataja kuwa ni pamoja na Bayport Tanzania, Barick Gold Tanzania, Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT-MD).
Akizungumza katika hafla hiyo Askofu wa KKKT wa Dayosisi ya Mwanga Askofu Chediel Sendoro, alimpongeza Bi Jennifer, kwa ubunifu wake ambao alisema utachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Maktaba hii ijapokuwa ipo kwenye jengo la Kanisa itatumika kwa watu wote bila kujali imani zao za kidini, lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kujiendeleza na kupata maarifa ya ziada kwa ajili ya maendeleo yake binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema.
Aidha aliwapongeza wazazi wa Bi Jennifer Dickson na Dk. Linda Ezekiel, kwa malezi mazuri ya wazazi waliyompa binti yao ambayo yalimwezesha yeye (Jennifer) kuja na maono yenye lengo la kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Nichukue fursa hii kuwataka wazazi wengine kuiga mfano wa wazazi wa Jennifer; pia niwasihi watoto wengine kuiga mfano wa Jennifer ili taifa liendelee kupiga hatua kupitia vijana wetu”, alisema.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Bonaventure Rutinwa, amesema kuwa maktaba hiyo ni miundombinu ya kielimu inayomwezesha mtu wakiwemo watoto wadogo kupata elimu ya ziada kupitia usomaji wa vitabu, ambapo alisema ni vyema watoto wakaanza kusoma. kufahamishwa kuhusu umuhimu wa kutumia maktaba mapema katika hatua za utotoni.
“Tunasoma sio kupata elimu ya shule pekee bali kuboresha maisha yetu kwa ujumla na hii ni moja ya maana halisi ya kuwepo kwa maktaba kuwa;maktaba zimekusudiwa kwa ajili ya watu wote na si kwa ajili ya wanafunzi na walimu pekee”,alisisitiza.
Post A Comment: