ZIKIWA zimebakia siku chache kabla ya kufanyika mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon kwa mwaka wa 2024, waandaaji wa mbio hizo wametoa maelezo na maelekezo kuhusu kufungwa kwa baadhi ya barabara na shughuli kadhaa na hivyo kubadili mwenendo wa baadhi za shughuli katika manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa waandaaji hao, maelekezo hayo yanalenga kuwasaidia wakazi wa Moshi na wale wa maeneo ya jirani kupanga safari zao mapema na kutumia njia mbadala pale inapohitajika ili kutoa nafasi kwa mbio hizo zitakazofanyika Februari 26, mwaka huu kufanyika kwa usalama kama inavyotarajiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Barabara ya Sokoine kutoka kona ya KCMC hadi Barabara ya Kilimanjaro zitafungwa kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi, ambapo wenye magari wanashauriwa kutumia njia mbadala za kwenda katikati ya mji wa Moshi kupitia eneo la Shanty Town na kata ya Rau hadi eneo la Mweka lililoko Kibosho.
Pia Barabara ya Kilimanjaro hadi kona ya Barabara ya Sokoine inayoelekea hospitali ya rufaa ya KCMC itafungwa kuanzia saa 1:45 aubuhi hadi saa 3:30 asubuhi.
“Hatua hii itatoa fursa kwa washirki wanaofika eneo la kuanzia mbio hizo kupata maeneo ya maegesho katika viwanja vya shule ya polisi Tanzania (CCP) pamoja na eneo la lango kuu la chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU) lililoko barabara ya kuelekea Uru sambamba na kupata nafasi ya kutosha kwa washiriki wakati wa kuanza kwa mbio hizo”, ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, barabara ya Masoka hadi Mweka kupitia eneo la Kibosho pia itafungwa kuanzia saa 12:30 hadi saa 2:30 asubuhi.
Taarifa hiyo inasema pia hakutakuwa na maegesho katika Barabara ya Sokoine kutokea kona ya Barabara ya Kilimanjaro ambao taarifa hiyo imeonya kuwa gari lolote litakaloegeshwa eneo hilo litachukuliwa na maofisa wa polisi wa kikosi cha usalama barabarani.
“Kutakuwa na maegesho ya bure kwenye eneo la shule ya polisi CCP, ambapo wanaotaka kuegesha vyombo vyao vya moto wataingilia kupitia Barabara ya Kilimanjaro na eneo ambalo mbio za nusu marathon za Tigo (Tigo Half Marathon) zitaanzia.
Pia kutakuwa na maegesho ya bure kwenye eneo lenye kivuli kizuri katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) ambalo linaweza kufikiwa kwa kupitia barabara inayoelekea Uru tu; ene hilo ni mwendo wa dakika tano tu kutoka uwanjani hadi eneo ambapo mbio za kilomita tano na zile za kilomita 21 zitaanzia na dakika mbili kutoka pale za kilomita 42 zitaanzia.
“Jeshi la Polisi kupitia kikosi chake cha usalama barabarani linatarajiwa kudhibiti maswala yote ya barabarani katika barabara zote kuanzia muda wa saa 12 asubuhi hadi saa 6:30 mchana, ambao madereva wameshauriwa kuwa waangalifu na makini ili kuhakikisha usalama wa washiriki wa mbio hizo”, ilisema taarifa ya wandaaji, ambapo pia walitakiwa kuepuka kutumia barabara ambazo zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya mbio hizo ili kuepuka changamoto zinazoweza kuwapata kwa kukiuka maagizo hayo.
Wakati huo huo, zoezi la ukusanyaji wa namba na vifaa kwa ajili ya ushiriki wa mbio hizo mwaka huu, umeanza Alhamisi 22 hadi 24 mwaka huu katika Uwanja wa Ushirika.
Mgeni rasmi katika mbio hizi za Jumapili ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro.
Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager kilomita 42km, kilomita 21 za Tigo (Tigo Half Marathon) kilomita tano za kujifurahisha chini ya udhamini wa Gee Soseji, wadhamini wa meza za maji TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na CRDB Bank. Wabia rasmi ni CMC Automobiles, GardaWorld Tanzania na Salinero Hotel. Wasambazaji rasmi ni Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.
Share To:

Post A Comment: