Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Phillip Mpango amezindua uuzaji wa Hati fungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) yenye thamani ya Sh Bilioni 53.12 kwa kusema kuwa kitendo cha mamlaka hiyo kutafuta uwezeshaji wa kifedha mbadala ni kitendo cha kuigwa na tassisi zote nchini.
Dk Mpango ambaye awali leo aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Kuboresha Hali ya Upatikanaji wa Maji jijini Tanga na Wilaya ya Mkinga wenye thamni hiyo ya Sh Bilioni 53.12 alisema kitendo cha mamlaka hiyo kuamua kutafuta uwezeshaji mbadala ya fedha ni kitendo cha maendeleo.
“Sasa hivi fedha za msaada zimekauka kwa sababu wenyewe wanaotoa misaada wana matatizo yao. Mikopo ina mashahrti magumu,hivyo lazima tutafte njia mbadala,” alisema.
Alisema uwezeshaji mbadala kutumia hati fungani ni njia sahihi kabisa ambayo inahakikisha watanzania kutumia fedha za ndani kwa ajili ya kugharamia murado ya maendeleo,
Alimsifia Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye alikutana na Mfuko wa Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNCDF) na kuridhia kutumika kwa hati fungani kwa serikali za mitaa na taasisi za serikali katika uwezeshaji wa mradi ya maendeleo. “Hii ndiyo njia ya kwenda. Naipongeza Tanga UWASA kuwa namba moja katika ngazi ya taasisi,” alisema Dk Mpango.
Alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na ukweli kuwa mpango wa serikali una uhitaji makubwa ya fedha na kutoa mfano wa sekta ambayo alisema zinahitajika raslimali fedha kubwa kuondoa kero ya maji nchini.
Aliipongeza UNCDF kwa kufadhili na kuratibu mchakato mzima wa hati fungani na kupongeza Bunge kwa kuwa mstari wa mbele wa kuishauri serikali kutafuta vyanzo mbadala vya fedha.
Hata hivyo, alitahadharisha Tanga UWASA kuhakikisha kuwa utekelezaji wa uuzaji wa hati fungani hauathiri utendaji na utoaji huduma au kuathiri bei ya maji kwa watumiaji9.
Pia Dk Mango alionyesha kukerwa na taarifa ya madeni ya maji ambayo taasisi za serikali zinadaiwa na Mamlaka za maji na kuagiza wizara ya Maji kuorodhesha taasisi ambazo zinazodaiwa na kuiwakilisha kwa Wizara ya Fedha ili ziwe zinakatwa wakati wizara hiyo inapopeleka fedha katika taasisi hizo.
Alisema hata hivyo ukataji fedha huo uwe na tahadhari hususan taasisi za ulinzi na afya ambazo alisema zina umuhimu katika kuhudumia wananchi.
Naye Afisa Mtedaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama alisema kuwa kitendo cha Tanga UWASA kutumia hati fungani kimeiweka Tanga katika ramani ya masoko ya mitaji duniani.
Aliisifu Mamlaka hiyo kwa kuionyesha njia mbadala ya uwezeshaji wa miradi na kuzitaka taasisi nyingine kutumia njia hiyo ya hati fungani ili kutekeleza mipango ya kwapa maji wataanzania.
Alisema kuwa taarifa za awali za uuzaji wa hati fugani zinaonyesha kuwa zimepita kiwango na kusema kuwa Tanga UWASA kmeonyesha njia kwa mamlaka nyingine katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Wakati umefika kwa taasisi na mashirika ya serikali kusimamia nafasi zao na kichocheo cha maendeleo nchini,’ alisema Mkama.
Naye Waziri wa Maji, Jumaa Awesso alisema tukio la kuzindua uuzaji wa wa hati fungani ya kijani miundombinu ya Maji ni wa kihistoria katika uwezeshaji wa miundombimu ya maji nchini na miradi mingine ya maendeleo.
“Hili ni jambo jipya. Tunampogeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa kulifanya jambo hili kuwa jepesi. Tuliliona ni gumu lakini tulipolipeleka kwake likuwa rahisi. Kweli Raisi Samia ni suluhu ya matatizo yetu,” alisema Aweso.
Alisema kuwa hii ni fursa. Fursa ikigonga haifai kuifungia milango. Tutashirikiana na wadau wote kwa ajili ya maendeleo,” alisema na kuongeza kuwa katika nchi zenye maendeleo kuna mchango mkubwa wa sekta binafsi.
Awesso alisema kuwa huu ni muda muafaka kwa mamlaka za maji kujitegemea na akaeleza kuwa mafanikio watakayopata Tanga UWASA yatafungua milango kwa taasisi nyingine kuwekeza katika uuzaji wa hati fungani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mhandisi Geoffrey Hilly alisema kuwa maombi ya kupata fedha kwa ajili utekelezaji wa mradi huo yalikaa kwa miaka 10 bila kupata wafadhili lakini walimua kutumia fursa ya uuzaji wa hati fungani ili kutekeleza mtradi huo ambao ni muhimu katika kuboresha huduma za maji kwa jiji la Tanga, sehemu za wilaya ya Muheza na wilaya ya Mkinga.
Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia lita milioni 60 kwa siku kutoka milioni 45.
Post A Comment: