315a7363-b952-4ff8-a482-54a348ef350f


Na Ashrack Miraji


Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameagiza Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani humo kutumia ubunifu, weledi pamoja na busara katika kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waadilifu.


Mkuu huyo wa wilaya amebainisha hayo katika kikao cha kamati ya ushauri wa kodi cha wilaya na kusisitiza kuwa mfanyabiashara yeyote atakaye bainika kuendelea kukiuka kulipa kodi taarifa iwasilishwe Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


Amesema suala la ulipaji kodi ni wajibu wa kila mwananchi kisheria ili kusaidia Serikali kupanga shughuli za kuwaletea wananchi wake maendeleo, akihimiza TRA kuwa wabunifu katika ukusanyaji mapato na kufanya operesheni za mara kwa mara kwa wafanyabiashara wote wilayani humo.


“TRA fanyeni operesheni za mara kwa mara kwa wafanyabiashara wote ambao wapo ndani ya wilaya ya Same na wanaostahili kutumia mashine za Kielektroniki (EFD) basi wanakuwa nazo na kwa wale ambao watakuwa wakaidi baada ya kuwafuatilia na kuwapa elimu basi sheria iweze kuchukua mkondo wake juu yao kwani hao ni wahujumu uchumi wa serikali”.


Kwa upande wake meneja wa TRA wilaya ya Same Eliapenda Mwanri amesema ufanisi  wa utendaji unatokana na ziara za mara kwa mara za mkuu wa wilaya na kamati yake ya usalama ya kuwatembelea wafanyabiashara katika biashara zao kusisitiza utoaji wa risiti za kielektroniki, ulipaji wa kodi kwa wakati pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto za  kibiashara, pia kupata maoni ya kuboresha biashara zao.


Kwa mwaka wa fedha 2023/24 TRA wilaya ya Same imekusudia kukusanya shilingi bilioni 4. 6 (4,637,450,937.77) sawa na ongezeko la asilimia 48% ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2022/23 ambapo lengo lilikuwa ni shilingi bilioni 3.6 (3, 685, 320, 179.62).


Katika kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Februari 2024 imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 2.2 (2, 240, 762, 028. 53) sawa na ufanisi wa asilimia 74.2% ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 3.0 (3, 021, 651, 706. 79. na makusanyo haya sawa na ongezeko la asilimia 8.2 ikilinganishwa na kipindi kama hiko mwaka 2022/23 ambayo yalikuwa Shilingi Bilioni 2.0 (2, 070, 285, 159. 60).


0ad179c7-ea82-41df-a95e-0526cc6d9b41

33a45fc0-5a96-43e9-bad3-774b98079df3

cbf13f26-7929-4443-8e86-047e42333a5c
Share To:

Post A Comment: