Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) Christine Mwakatobe akiwa mwanamke wa kwanza kuongoza taasisi hiyo  tangu kuanzishwa mwaka 1978, ametaja kipaumbale chake kitakuwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato vinavyoliingizia taifa fedha za kigeni kwa kuvuta mikutano zaidi ya kimataifa. 

Mwakatobe alitaja mkakati wake huo ambapo kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya tano katika Afrika kwa ufanyikaji wa mikutano ya kimataifa ikiwa nyuma ya Afrika ya Kusini, Morocco, Rwanda na Misri. 

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Arusha  mwishoni mwa  wiki ikiwa kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kuongoza taasisi hiyo Machi 18 Mwaka huu, Mwakatobe alisema mkakati wake huo umelenga katika kutoa gawio la kutosha kwa serikali

"Sitamwangusha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani nami na kuniteua kuwa mtendaji mkuu wa taasisi hii muhimu kwa uchumi na diplomasia ya nchi, " alisema. 

Alisema lengo ni kuifanya AICC  kuwa kitovu cha mikutano kwa eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kwa kuendeshwa  kisasa ikijumuisha matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza uwezo wa kuandaa mikutano ya kimataifa. 

Kwa upande wake aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC Ephraem Mafuru alisema mpango mkakati wa mwaka wa fedha 2023/2024 ni  kuwa na Kituo kikubwa zaidi cha mikutano jijini Arusha. 

Mafuru ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Nchini(TTB) alisema kituo hicho kitaitwa Mount Kilimanjaro Convention Centre kitachokuwa na eneo la washiriki 10,000, maduka makubwa pamoja na hoteli mbili za nyota tano. 

Licha ya kuendesha shughuli zake  jijini Arusha, lakini AICC ambayo kwa mwaka wa fedha uliopita iliingiza mapato ya shilingi bilioni 18.7 pia inaendesha kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam. 

Katika mwaka huu wa fedha AICC inatarajiwa kuingiza mapato ya shilingi bilioni 23.

Kabla ya uteuzi huo,  Mwakatobe alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akipanda kutokea kuwa Meneja wa mipango na biashara. 

Alichukua wadhifa huo akiwa mwanamke wa kwanza  kupanda ngazi mpaka kushika usukani katika uwanja huo uliokuwa ukiendesha na Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja wa Ndege Kilimanjaro(KADCO)  tangu ulipojengwa mwaka 1971.

KIA iliweza kuongeza idadi ya mashirika ya ndege yanayotumia uwanja huo na kufikia 15 pamoja na usafirishaji wa shehen na kuwa  jumla ya tani 4,426.3363 kwa mwaka wa 2022 kutoka tani 3,271.787 mwaka wa 2019.











Share To:

Post A Comment: