WAJUMBE wa Kamati ya Siasa ya chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro wameitaka serikali kutowapa kazi wakandari ambao wamekuwa wakichelewesha ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa barabara wilayani humo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kutembelea barabara ya Kiboroloni – Kidia yenye urefu wa kilomita 1 inayogharimu zaidi ya millions 824 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ilitakiwa kukamilika mwezi Juni mwaka jana lakini mpaka sasa haijakamilika na kuongezea muda hadi Aprili mwaka huu na mkandarasi akiwa ni Ngenda construction.
Akizungumza Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi vijijini, Ramadhani Mahanyu alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani imekuwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Mahanyu alisema kuwa, wapo baadhi ya wakandari ambao ni wazembe wamekuwa wakikwamisha juhudi hizo za Rais na kuitaka serikali kutowafumbia macho wakandari wazembe ambao wamekuwa hawakamilishi miradi kwa wakati.
“Ifike mahali wakandarasi wazembe ambao hawafanyi kazi kwa weledi msiwape kazi katika wilaya yetu maana watu wa namna hii wanachonganisha chama na wananchi wake na sisi hatupo tayari kwenye hili” Alisema Mahanyu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi alisema kuwa, barabara hiyo imekuwa kero kubwa kwa wananchi hasa kipindi cha mvua.
Ndakidemi alitumia nafasi hiyo kuwaomba Wakala wa barabara nchini Tanroad ambao ndio wasimamizi wa barabara hiyo kuwa wakali kwa mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili kuhakikisha anafanya kazi na kukamilisha kwa wakati uliowekwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori aliitaka Tanroad kumwandikia barua za unyo mkandarasi huyo na pindi akiendelea na ucheleweshaji wa mradi huo waanze kumkata fedha za ucheleweshaji mradi.
Alaisema kuwa, wakandarasi wazembe hawana nafasi katika wilaya ya Moshi na kutaka mkandarasi huyo asipewe kazi nyingine katika wilaya ya Moshi.
Awali akisoma taarifa za ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Tanroad mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando alisema kuwa, mpaka sasa mkandarasi huyo amefikia asilimia 30 za ujenzi wa barabara hiyo.
Mhandisi Motta alisema kuwa, mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa milioni 258 kwa kazi ambazo ameshazifanya na kuongeza kuwa mkandarasi huyo amekuwa akisuasua katika ujenzi wa barabara hiyo.
Post A Comment: