Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Jiji la Tanga, limepokea na kupitisha rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025, katika kikao kilichohudhuriwa na Menejimenti, Wawakilishi wa Wafanyakazi kutoka Idara na Vitengo, pamoja na Viongozi kutoka Vyama mbalimbali vya Wafanyakazi.

Baraza hilo lililoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Wakili Sebastian Danda, lilitanguliwa na uchaguzi wa viongozi wa Baraza, ambapo Wakili Idrisa Mbondera alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza kwa miaka mitatu, huku Bi. Aisha Toba akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza.

Katika nafasi za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza, walichaguliwa wajumbe watatu kuwakilisha Idara na Vitengo vya Jiji la Tanga, ambapo wajumbe hao ni pamoja na Salim Mzee (Kitengo cha Fedha na Uhasibu), Farida Hatim (Idara ya Maendeleo ya Jamii) na Hussein Mbwana (Idara ya Biashara).

Akizungumza kabla ya uchaguzi, Afisa Kazi Msaidizi, Ofisi ya Kazi Mkoa, Bi. Edithstella G. Mbezi, ambaye ndiye aliyekuwa Msimamizi wa uchaguzi huo, amesema Baraza la wafanyakazi ni muhimu katika uendeshaji wa ofisi au taasisi kwa kuwa linatoa nafasi ya kushirikisha na kushauri maslahi ya Wafanyakazi, kanuni za Utumishi, na kwamba linapaswa kukaa vikao viwili kwa mwaka, ambapo katika kikao cha kwanza ni cha mipango na bajeti, na cha pili kikiwa ni cha tathmini ya utekelezaji.

Kufanyika kwa kikao maalum cha Baraza la Wafanyakazi kupitia rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2024/2025, ni muendelezo wa ratiba ya vikao vya kisheria vinavyofanyika katika kukamilisha mchakato wa upitishaji wa Bajeti katika ngazi ya Halmashauri.

Share To:

Post A Comment: