Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia S. Hassan ametuma salamu za pole kwa wachimbaji mkoani Simiyu kufuatia vifo vya zaidi ya wachimbaji 21 waliofukiwa na kifusi katika kijiji cha Ikinabushi,Wilayani Bariadi-Mkoa wa Simiyu.

Salamu hizo zimetolewa leo Kijijini Ikinabushi,Wilayani Bariadi-Simiyu na Waziri wa Madini  Anthony Mavunde wakati akizungumza na wachimbaji katika eneo hilo na kuwasilisha salamu za pole za Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa ndugu,jamaa na familia zilizopoteza wapendwa wao kufuatiwa kufukiwa na kifusi wakati wa zoezi la uchimbaji.

Waziri Mavunde amesema eneo hilo la uchimbaji kwa sasa litasimama shughuli za uchimbaji mpaka ambapo Wizara kupitia kitengo cha Ukaguzi Migodi na Mazingira kitakapojirdhisha juu ya usalama wa eneo hilo kiuchimbaji ndipo itaruhusu shughuli hizo ziendelee.

Akaongeza pia,kufuatia maombi ya wachimbaji hao zaidi ya 500 kuomba kuendelea na uchimbaji wa eneo hilo kwa lengo la kujitafutia riziki,Mh. Rais ametoa maelekezo kwa Wizara kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili wachimbaji hao warasimishwe na kupatiwa Leseni ya madini.

Katika hatua nyingine,Waziri Mavunde amewataka wachimbaji hao waunde kikundi cha pamoja ili kupatiwa Leseni na kuzitaka mamlaka za Mkoa na wilaya kusimamia zoezi hilo.

Akizungumza katika mkutano huo,Mbunge wa Jimbo la Bariadi Eng. Andrea Kundo ameishukuru serikali kwa kuwakimbilia kwa uharaka kutokana na majanga yaliyotokea na pia kutumia fursa hiyo kumshukuru Mh Rais kwa hatua ya upatikanaji wa leseni kwa kuwa wananchi hao shughuli yao kubwa ya kiuchumi ni uchimbaji na ndio maisha yao.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda amevishukuru vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga kwa kusimamia vyema zoezi la kutoa miili na kuimarisha usalama katika eneo hilo na kwamba kwasasa atasimamia kuhakikisha shughuli zinasimama kwanza mpaka taratibu za kiusalama kukamilika.

Share To:

Post A Comment: