Serikali kupitia Wizara ya Madini imewahakikishia wafanyabiashara ya Madini mkoani Arusha kuwa ipo tayari kutatua changamoto zote zinazowakabili wafanyabiashara wa madini mkoani humo.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati wa ziara ya kikazi mkoani Arusha alipotembelea masoko ya madini katika eneo la Uzunguni.

Akizungumza na wafanyabiashara hao mapema baada ya kupokea taarifa ya mwenendo wa biashara ya madini mkoani humo kutoka kwa Mwenyekiti wa Soko la Madini Abost Mollel, Katibu Mkuu Kheri Mahimbali amefafanua kuwa Serikali inatambua kuhusu changamoto hizo na ipo katika hatua mwisho za utatuzi ambapo hivi karibuni tamko litatolewa.

Kwa upande wake, Mweyekiti wa Wafanyabiashara Soko la Madini Arusha Abogast Mollel amesema kuwa hivisasa biashara ya madini imekuwa ngumu kutokana na soko la madini kuhamishiwa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara jambo ambalo limesababisha wafanyabiashara wengi wa madini ya Tanzanite kufunga biashara zao.

Akielezea kuhusu mwingiliano wa biashara katika soko moja, Mollel amesema kwamba hivisasa wanashindwa kupata takwimu sahihi za mauzo na manunuzi ya madini kutokana na mwingiliano wa wafanyabiashara na wanunuzi kuwa katika eneo moja jambo linalopelekea kutokupatikana kwa usahihi wa taarifa.

Naye, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini ya Vito Tanzania Osman Tharia ameishukuru Serikali kwa kufanya ziara katika eneo la soko na kwamba anaamini kwa kufanya hivyo kutatoa picha halisi ya hali inayoendelea katika masoko hayo na kupata njia sahihi za kuweza kutatua changamoto hizo.

Akielezea kuhusu leseni moja kutumika eneo hilohilo, Tharia ameiomba Serikali kubadilisha mfumo kwani kuwa na leseni isiyovuka mipaka ni kuwafungia fursa katika maeneo mengine yenye fursa kama hizo.

Awali, Katibu Mkuu amekitembelea Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) kinachotoa mafunzo ya kuongeza thamani madini ambapo alipata kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Maabara ya Madini Vito.

Share To:

Post A Comment: