Na John Walter-Manyara

Imeelezwa kuwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi katika halmashuri ya mji wa Babati kimepungua kutoka asilimia 2.6 kwa mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 1.8 kwa mwaka 2023.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Nakwa kilichopo kata ya Bagara wilayani Babati mkoani Manyara, afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya mji wa Babati Diana Bakari Mchonga amesema juhudi za kutoa elimu kwa jamii zimesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza maambukizi.

Aidha amesisitiza waliopata maambukizi kuendelea kutumia dawa na kujiamini kwani kuacha kutumia dawa kutaongeza changamoto kubwa zaidi ya kiafya hata kupelekea kifo.

Mchonga amefafanua bayana mikakati waliyoweka ya kuendelea kupambana na janga hili la ukimwi ikiwa ni kuongeza juhudi za kutoa elimu zaidi kwa jamii kwa kufanya mikutano ya hadhara na kuwatembelea nyumba kwa nyumba.

Kwa upande wa shuhuda Bi Hadija Matola ameelezea alivyopata maambukizi na kuwasihi kina mama kuwa mastari wa mbele kukabiliana na changamoto hiyo hasa wakati wa ujauzito.

Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani hufanyika kila ifikapo tarehe moja (1) Disemba ya kila mwaka na kwa mwaka huu kauli mbiu inasema “jamii iongoze kutokomeza ukimwi”.

Share To:

Post A Comment: