Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimewakutanisha wadau wa TEHAMA ndani na nje ya mkoa wa Arusha kujadili masuala mbalimbali kuhusu TEHAMA na uanzishwaji wa mitaala bora ilikuweza kutoa wataalam wenye uwezo na ujuzi, huku kauli mbiu ikiwa  "Mabadiliko ya kidigitali katika kuendeleza shughuli za binadamu ".

Akizungumza katika Kongamano hilo Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka  amesema Kongamano hilo limekuwa chachu katika kuibua vipaji kwa wanafunzi, kuonesha kazi zao za ubunifu na uvumbuzi katika TEHAMA, kuwakutanisha na wadau wa TEHAMA na kujadiliana namna ya kuwawezesha  kuweka mazao ya ubunifu wao sokoni.

“Sisi kama Chuo tumewekeza katika miundombinu ya TEHAMA, mitaala na rasilimaliwatu; IAA kupitia Mradi wa HEET tunatarajia kujenga kituo cha kikubwa cha umahiri cha TEHAMA, ambapo mtu yeyote atakayehitaji suluhisho la changamoto yoyote ya TEHAMA atakuja IAA,” amesema Prof.Sedoyeka.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi Mhandisi. Jasson Ndanguzi amesema, Tume hiyo itaendelea  kushirikiana na Vyuo vya elimu ya juu katika kufanya tafiti zinazoibua mwelekeo wa TEHAMA, zinazotatua changamoto za jamii, kuibua fursa za kiuchumi pamoja na kuiwezesha serikali kuandaa sera zinazoendana na wakati.

Mhandisi Ndanguzi ameipongeza IAA kwa  kufanya makongamano ya TEHAMA na kuahidi kuwa Tume itaendelea kuwasaidia wabunifu wa mifumo ya TEHAMA hususani wanapofikia hatua ya kuipeleka mifumo yao sokoni kwa walaji ili watimize lengo la kuisaidia Jamii.

Hata hivyo Amidi wa Kitivo cha TEHAMA katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Edson Lubua amesema kongamano hili limekuwa likitoa motisha kwa wanafunzi na kuonesha thamani ya kazi za ubunifu pale wanapozionesha kwa walaji ambao ni makampuni, waajiri na taasisi mbalimbali ambazo zinaweza kuwawezesha kufikia ndoto zao.

Vile vile wanafunzi wa shahada ya usalama wa mtandao, ambao wamebuni mfumo maalum wa kutengeneza vitambulisho,  unaoweza kutumika na taasisi mbalimbali, hivyo wametoa wito kwa wamiliki na wakuu wa taasisi kuwaunga mkono kwa kutumia mfumo huo ambao kwa sasa unatumika kutengeneza vitambulisho kwa wanafunzi wote wa IAA.

Pamoja na mfumo wa kutengeneza vitambulisho wametengezeza mifumo mingine mbalimbali waliyoionesha katika kongamano hilo ikiwemo mfumo wa utambuzi wa magonjwa katika mimea, mfumo wa utafutaji wa mafundi kupitia mtandao pamoja na mfumo wa utoaji wa taarifa katika taasisi kupitia mtandao.















Share To:

Post A Comment: