ZAIDI Sh milioni 413.923 zimetolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ya ukamilishaji wa majengo saba ikiwemo miundombinu kwenye Chuo cha  Ualimu Ngorongoro

Fedha hizo zimetolewa kupitia mradi wa ESPJ II, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ametembelea chuo hicho na kujionea uhalisia wa ujenzi wa chuo hicho kilichokamilika kwa asilimia 85.

Kwa mujibu wa Kaimu Mdhibiti Ubora wa Elimu wilayani Ngorongoro, Godfrey Mtune, jengo la utawala, jengo la mkuu wa chuo,nyumba ya wakufunzi, maktaba, bweni la wasichana na wavulana na madarasa yapo kwenye hatua za mwisho za umaliziaji.

Amesema hivi sasa jengo hilo lipo hatua za kufanya marekebisho kwenye mifumo ya maji safi na maji taka, kupaua bweni moja, kupiga mbao katika bweni la wavulana upigaji plasta ndani na nje ya jengo ikiwemo maboresho mbalimbali.

“Ujenzi wa chuo hiki umefikia asilimia 85 lakini mabadiliko ya bei za bidhaa za viwandani kutokana na bei za mafuta kupanda zinaathiri mradi huu kwa kiasi ikiwemo bei za saruji,” amesema.

Naye RC Mongella amesema kukamilika kwa ujenzi wa chuo hicho kutaleta taswira ndani ya wilaya hiyo na kusisitiza kasi ya ujenzi iongezwe, kwani  mkataba wa ujenzi wa majengo hayo unatakiwa kukamilika Novemba 30 ,mwaka huu.

Share To:

Post A Comment: