Uwekaji wa miundombinu ya maji taka uliofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (Auwsa) umepelekea baadhi ya barabara za Jiji hilo kutengeneza mashimo makubwa kusababisha maji ya mvua kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Kadhia ya maji hayo kuvamia makazi ya wananchi mtaa wa Msasani Kata Murriet umepelekea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella kutoa siku tatu na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Auwsa, Mhandishi , John Ndetico kurekebisha miundombinu hiyo mara moja kuanzia jana ili kuondoa changamoto ya maji kuingiza kwenye makazi ya watu.

“Hivi wataalam huwa mnafanya nini mnaposimamia miradi hebu angalieni mlichokifanya ,mmechimba mtandao wa maji taka halafu barabara mkaifukia kienyeji badala ya kufukia kitaalam sasa mvua zimenyesha udhaifu wenu umeonekana,mlikuwa mnasimamia nini”

Ameagiza Auwsa kukagua maeneo yote waliyopitisha miundombinu hiyo ya maji taka iliyoharibu barabara na kutengeneza upya kwa viwango vinavyotakiwa na kusisitiza kuwa atapita usiku na mchana kukagua ili ajiridhishe.

“Wazazi na walezi muwe makini kuangalia watoto wenu wasije kuzama maana barabara zimetitia muwe makini ili maafa mengine yasije tokea”

Naye Mhandisi Ndetico amesema mkandarasi aliyepewa mradi huo,Sinohydro Corporation Ltd
alishamaliza muda wake hivyo Auwsa itafanyia kazi changamoto hiyo ili tatizo hilo lisiweze kujirudia tena.

Awali Mwenyekiti wa Mtaa wa Msasani,Rashid Chidi na Anna John wamesema kuwa wakati Auwsa wanachimba mifumo wa maji taka walieleza changamoto ya barabara kuharibika lakini waliambiwa waache kuingiza siasa katika masuala ya utaalamu ila kwakuwa mvua zimenyesha na zimeonyesha tatizo hilo sasa watalifanyia kazi kwani barabara zimegeuka mahandaki na wakati mwingine kuhatarisha usalama wa watoto wadogo, watu wazima na watu wa rika mbalimbali.

Share To:

Post A Comment: