Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Uhasibu Tanzaia (TIA), Kampasi ya Singida imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanafunzi wapya wa Taasisi hiyo walioanza msimu wa masomo 2023/
2024 kwa lengo la kuwaandaa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa soko la ajira
baada ya kumaliza masomo yao.
Akizungumza Novemba 16, 2023 kwenye mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Mpango wa Uendelezaji wa Vipaji na Ajira kwa Vijana wa Taasisi hiyo nchini, Imani Matonya alisema Taasisi ya Uhasibu Tanzania
imeanzisha mpango huo kwa malengo matatu moja likiwa ni kuwajengea uwezo
wanafunzi na kuwasaidia kupata mbinu za kitaalam ambazo wanatakiwa kuwa nazo
zaidi ya taaluma waliosomea.
Matonya alitaja lengo la pili ni kuwafundisha wanafunzi hao mbinu za kuwa
wajasiriamali bora kwa kuwaruhusu kuonesha biashara mbalimbali wanazozifanya
bila kujali ukubwa wa biashara hiyo hata kama watakuwa wanauza ubuyu.
"Sisi tunaamini ujasiriamali ni tabia na maarifa na ndio maana kuna
baadhi ya watu wanatuambia inakuwaje tunafundisha masuala ya ujasiriamali
lakini hatujishughulishi nao ndio maana utakuta kuna mtu hajasoma lakini ni
mbobezi katika ujasiriamali," alisema Matonya.
Alisema jambo la tatu wanalolifanya ni kuchagiza ubunifu ili wanafunzi
waweze kuja na utatuzi wa kitaalam kwenye mambo ya msingi yanayolikabili taifa
letu na kuwa jambo la nne wanafanya uhatamizi wa mawazo bunifu mwanafunzi akiwa
na wazo fulani la biashara wanampa nafasi ya kulihatamia na kumsaidia bure
kupata usajili na mahitaji mengine kama ya kupata mwanasheria muhuri wa chuo
hivyo kumrahisishia mambo yake,
Alisema kupitia mpango huo wamejipanga kutoa mafunzo hayo mara kwa mara
kwa ajiliya kuwajengea uwezo wa kupata mawazo ya biashara ambayo yatawasiadia
katika kujiajiri.
Alisema wanafunzi wenye mawazo mazuri watashindanishwa na mawazo
yatakayoshinda yatapelekwa mbele zaidi kwa kutafutiwa mitaji na kukutanishwa na
taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo ya kuanzisha biashara.
"Leo tumekuja Singida kuwaelekeza vijana kuhusu maisha yao kwa ujumla
na kuwapa hamasa kwamba wanaweza kuwa bora na kuwajuza mambo mawili la kwanza
ni suala la kujiajiri kupitia ubunifu na ujasiriamali na kuwafundisha namna ya
kuandika mipango biashara inayoshinda ambayo watafundishwa na watu kutoka
mitaani wenye ujuzi wa hayo mambo na wanayafanya kwa vitendo," alisema
Matonya.
Alisema watu hao watawaeleza kwa vitendo na kuwapa chagizo la kuweza
kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ya kuomba ufadhili na kuwafanya wawe na
ujasiri wa kusimama mbele ya wawekezaji kuwaomba waweke uwekezaji kwenye miradi
yao.
Alisema vijana wengi wanamawazo mazuri na biashara nzuri lakini changamoto
waliyonayo wameshindwa kuwavutia wawekezaji kwa sababu hawana mbinu za
kuwasilisha wazo mbele ya watu wenye fedha na kuona kama mawazo yao yana tija
kwa siku za usoni.
Matonya alisema lengo lingine la mpango huo ni kuwataka wanafunzi hao
nini wategemee kutoka kwenye soko la ajira kwani wapo watakao jiajiri lakini
kwa wale watakao taka kuajiriwa wanapaswa kuwa na vitu vya ziada ili iwe rahisi
kupita kwenye usaili na kuchaguliwa kuingia katika ajira.
Alisema leo hii ikitangazwa nafasi moja ya ajira watajitokeza watu kuanzia
100 hadi 200 kuigombea nafasi hiyo hivyo ni lazima mgombea awe na vitu vya
ziada ambavyo TIA wanavifundisha.
Naye Mwalimu wa Stadi za Mawasiliano na Lugha ya Kiingereza kutoka Chuo cha
Utumishi wa Umma Singida Eliasi Mchomvu alisema hivi sasa soko la ajira
limekuwa na changamoto ndio maana wapo TIA kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi
hao mbinu za kufanya vizuri wanapofanyiwa usaili.
Alisema hivi sasa lugha ya kiingereza imekuwa ndiyo ya ajira lakini
changamoto iliyopo watu wengi hawana uwezo mzuri kwenye lugha hiyo ambapo
walifundishwa mbinu ambayo itawasaidia kuijua vizuri na kuwa wakati wanaomba
kazi kuna baadhi ya vitu ni muhimu kuvizingatia.
Alisema jambo la kwanza wanapaswa kulisoma tangazo la kuomba kazi vizuri na
hapo ndipo watapata muongozo wa kuomba hiyo kazi yenyewe na mtu atakayekuwa
akifanya usaili atajua kuwa mwombaji ni mtu anayeelewa hivyo ni muhimu kuitwa
kwenye usaili.
Alisema jambo la pili ni muombaji kuandika wasifu wake ambapo mtu akiusoma
atajua aliyeuandika ameandika vitu vya msingi hivyo anafaa kuitwa kwenye
usaili.
Mchomvu alitoa angalizo katika uandikaji wa wasifu wake kuwa ni vema
akaandika maneno machache ya msingi badala ya kuandika maneno mengi ya
kujisifia kwani ndio utakaoleta maswali mengi wakati wa mahojiano ya hana kwa
hana na wasaili.
Aidha Mchomvu alishauri viandikwe vitu vya msingi ambavyo muombaji ataweza
kuvijibu kwa ufasaha wakati wa mahojiano ya ana kwa ana kwani mara nyingi
huwa inatokea mwombaji kuandika maneno mengi na wakati wa mahojiano anashindwa
kuyatolea ufafanuzi.
Akielezea mtu anayeandikwa pale chini kuwa wanaweza kuwasiliana naye kwa
maana anajua taarifa za muombaji wa kazi ' Refer ' alisema anatakiwa kuwa ni
mtu mwenye vitu vya ziada vya muombaji ambavyo havipatikani kwenye vyeti wala
kwenye wasifu wake na havitakuwepo mezani kwa watu wanaomfanyia usaili na amjue
kwa undani muombaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ksa arts and Decors Company, Allen Kazungu
alisema licha ya kuwa mwanafunzi katika Taasisi hiyo akishirikiana na wenzake
wawili waliweza kutumia jukwaa la shule kama fursa ya kuweza kupata mafunzo na
kujiendeleza na kuweza kufungua kampuni hiyo.
Alisema mwanafunzi akiwa chuoni anapata fursa ya kushiriki majukwaa
mbalimbali kiurahisi na bure na akitoka nje anaweza kuilipia kuanzia Sh.100,000
hadi 200,000 hivyo aliwashauri wanafunzi hao na vijana wengine popote pale
walipo kwa hali na mtaji wowote walionao wanaweza kuukuza wakiwa chuoni kupitia
walimu wa programu hiyo na kufungua kampuni zao.
Alisema kufungua kampuni na biashara ni jambo moja na kuwa vijana wengi wanakuja kukwama na kushindwa kuendelea kwa kukosa muelekeo na mipango thabiti hasa pale wanapokutana na changamoto badala ya kupambana nazo wao hukata tamaa.
Mkufunzi wa Stadi za Mawasiliano na Lugha ya Kiingereza kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Singida Elias Mchomvu, akitoa mada kuhusu usaili kwa wanaoomba nafasi za kazi.
Mkurugenzi wa Ksa arts and Decors Company, Allen Kazungu , akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Watoa mada wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Wanafunzi wapya wa TIA Kampasi ya Singida wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Watoa mada wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi (TIASO) wa taasisi hiyo Kampasi ya Singida.
Post A Comment: