Wananchi waendelea kuitika kwa shauku kubwa kushiriki michezo na kupata elimu ya uhifadhi wa misitu.
Bonanza la michezo linaloendelea katika Shamba la Miti Sao Hill limeendelea kushika kasi na kuleta hamasa kubwa kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mufindi na maeneo ya jirani ambapo bonanza hili limekuwa ni jukwaa muhimu la kuelimisha, kuburudisha, na kuunganisha jamii katika kampeni endelevu ya kulinda na kuhifadhi misitu.
Michezo hii imeendelea Oktoba 6, 2025 katika Tarafa ya Nne ya Shamba Mgololo ambapo imeshirikisha timu kutoka vijiji mbalimbali ambazo ni Lugala, Misitu FC, Mabaoni, Magunguli, Kitasengwa, Mpanga na Luhunga.
Fainali ya mchezo huu imechezwa kati ya timu ya Misitu FC na timu ya Luhunga ambapo timu ya Misitu FC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa penati 3 kwa 1 dhidi ya Luhunga baada ya mchezo huo kumalizika bila kufungana na hivyo kufanya timu ya Misitu FC kuwa mshindi wa jumla kwa upande wa tarafa ya Nne Mgololo.
Tangu kuanza kwake, michezo mbalimbali imekuwa ikiendelea kwa ushindani wa hali ya juu kwani timu kutoka vijiji vinavyopakana na msitu wa Shamba la Miti Sao Hill zimeonesha ari kubwa katika michezo kama mpira wa miguu, netiboli, kukimbia, kuvuta kamba, mashindano ya kula na kucheza draft ,na hivyo hali ya ushindani imekuwa ikichochea umoja na upendo baina ya washiriki huku furaha na shangwe zikitawala uwanjani.
Mbali na burudani, elimu kuhusu matumizi sahihi ya moto na njia bora za kulinda misitu imekuwa sehemu muhimu ya bonanza hili na Wahifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kutoa elimu hiyo kwa vitendo, wakisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mazingira.
Hii imekuwa ni fursa adhimu ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna tunavyoweza kutokomeza matukio ya moto misituni na washiriki na watazamaji wengi wameonesha kufurahishwa na ubunifu uliotumika katika kuandaa bonanza hili na wengi wamesema kuwa michezo hii si tu burudani, bali pia ni shule ya maadili, ushirikiano, na uwajibikaji katika kulinda rasilimali za taifa.
Bonanza limeendelea kuwa darasa la wazi linalounganisha michezo na elimu ya uhifadhi wa misitu na kadri siku zinavyosonga, idadi ya washiriki na watazamaji inaongezeka, jambo linaloonesha jinsi jamii inavyoitikia kwa moyo mmoja kwani watoto, vijana na watu wazima wamekuwa sehemu ya tukio hili, wakiendeleza ari ya ushiriki na kujifunza mambo mapya kuhusu utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa misitu.
Bonanza hili linaendelea leo Oktoba 7, 2025 katika Tarafa ya Pili ya Shamba Ihefu kwa kukutanisha timu mbalimbali zinazolizunguka shamba katika tarafa hiyo
Post A Comment: