Kiwanja cha Ndege  cha Kimataifa cha Kilimanjaro kimekabidhiwa rasmi kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) kutoka kwa iliyokuwa Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) baada ya  mkataba wa uendeshaji kukamilika novemba 9 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa hafla ya Makabidhiano ya Kiwanja hicho Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema pamoja na mabadiliko hayo yaliyofanyika Serikali itazingatia stahiki zote za Wafanyakazi zinalipwa kulingana na sheria.


“Kiwanja cha KIA ni Kiwanja cha kimkakati  hivyo pamoja na mabadiliko yaliyofanyika tayari kuna kikosi kazi kitakachohakikisha Viwango vya uendeshaji vinaendelea kukua na maslahi ya watumishi yanapatikana kulingana na Sheria za utumishi zilizopo’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa mabadiliko ya uendeshaji yaliyofanywa yanakwenda sanjari na maboresho katika usafiri wa anga yanayojikita katika ununuzi wa ndege mpya na ujenzi wa viwanja vya ndege ili kurahisisha shughuli za kibiashashara ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso amesema ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo iko chini ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na TAA inasimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amewahakikishia wadau wote kuwa pamoja na mabadiliko hayo huduma zitaendelea kutolewa kwa kuzingatia miongozo na kanuni za kimataifa zinazoongoza usafiri wa anga.

KADCO ni kampuni iliyosajiliwa 11 Machi 1998 kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 ambapo 06 Julai, 1998 Serikali iliamua Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kiendeshwe kupitia sekta binafsi ambayo ilikuwa kwa njia ya ubia kati yake na Kampuni ya Mott MacDonald ya Uingerereza, South African Infrastructure Fund ya Afrika Kusini na Kampuni ya InterConsult ya Tanzania) na mikataba miwili ambayo ni Mkataba wa Uendeshaji (Concession Agreement) pamoja na Mkataba wa Ukodishaji (Lease Agreement) baina yake na KADCO.


Mwaka 2010 kutokana na uendeshaji usioridhisha wa Kiwanja hicho Serikali iliamua kununua hisa za wanahisa wenza wa KADCO kwa kuvunja Mkataba wa Wanahisa na hivyo KADCO kumilikiwa na Serikali asilimia 100 ambapo iliendelea kuendesha KIA ikiwa ni Kampuni ya Serikali kupitia Mikataba ya Uendeshaji (Concession Agreement) na Ukodishaji (Lease Agreement) ambayo ukomo wake umefika mwisho tarehe 09 Novemba, 2023 , Serikali imeamua kuhamisha shughuli za Uendeshaji kutoka KADCO kwenda TAA.

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Uchukuzi)

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: