NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa barabara ya Ndevelwa-Igalula-Goweko anaanza kazi mara moja.

Mhe.  Ndejembi ametoa agizo hilo katika Kijiji cha Igalula wilayani humo wakati akizindua Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Igalula, Mhe. Venant Protas ambapo Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilipeleka kiasi cha Sh. Milioni Saba kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi hiyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mhe. Ndejembi amesema amepokea malalamiko kwamba mkandarasi aliyepewa mradi huo mpaka sasa bado hajaanza kazi licha ya kuwa alishasaini mkataba wa ujenzi zaidi ya miezi mitatu iliyopita.

"Nimesikia malalamiko kutoka kwa Mbunge kwamba Mkandarasi hayupo site licha ya kwamba ameshasaini mkataba muda mrefu tu. Ninamuagiza hapa Meneja wa TARURA Wilaya ya Uyui kuhakikisha mkandarasi huyu anaanza kazi haraka na kama hana uwezo basi atafutwe mkandarasi mwenye uwezo apewe kazi hii,"amesema.

Ameongeza "Hapa Wilaya ya Uyui pekee tumeleta kiasi cha Sh. Milioni 334 kwa ajili ya ukarabati wa barabara za TARURA takribani  barabara sita na hii barabara yenu yenye kilometa 52 ikiwa mojawapo."

Naye, Mbunge wa Jimbo hilo, Venant Protas amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh. Milioni Saba za kumalizia ujenzi wa ofisi hiyo ambayo imekaa muda mrefu tangu mwaka 2006 bila kukamilika.

Share To:

Post A Comment: