Mtendaji Mkuu wa AICC Bwana Ephraim Mafuru(Watano kushoto) akiwa katika picha ya Pamoja na kisha kuagana wachezaji wa timu ya AICC itakayo shiriki katika Michezo ya SHIMUTA Jijini Dodoma.

Na Freddy Maro AICC Arusha.

Mkurugenzi mkuu wa Kituo Cha Kimataifa Cha Mikutano Arusha AICC Bwana Ephraim Mafuru amesema michezo mahali pa kazi ina umuhimu mkubwa kwasababu inasaidia kuimarisha afya ya mwili na akili kwa wafanyakazi na inawapatia fursa ya kujenga mahusiano mema na wenzao kutoka tassisi nyingine.

Bwana Mafuru ameyasema hayo leo (11.11 2023) AICC Jijini Arusha wakati akiagana na timu ya michezo ya AICC inayokwenda Jijini Dodoma kushiri katika mashindano ya 52 ya michezo ya Taasisi za Umma na Mshirika Binafsi SHIMUTA inayoanza kesho.

“Napenda kuwapongeza kwa kupata nafasi ya kuiwakilisha taasisi yetu ya AICC katika michezo ya SHIMUTA, Ushiriki wenu na uwepo wenu katika michezo hii ni kielelezo tosha ya kwamba tuna dhamira ya kweli kutekeleza sera za Serikali ya awamu ya sita na hasa katika suala la michezo,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu Mafuru alisisitiza kuwa AICC imedhamiria kuboresha afya ya mwili na akili za wafanyakazi na kudumisha umoja ndani ya Kituo na kujenga mahusiano kati ya watumishi wa AICC na taasisi nyingine za serikali.

“ Kwa kutambua umuhimu wa kulinda afya za wafanyakazi wake dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanayoenea kwa kasi, AICC imejenga chumba cha mazoezi(Gym) na kununua vifaa vya kisasa ili kutoa fursa kwa watumishi kufanya mazoezi,” alisisitiza.

Kwa Upande wake kiongozi timu ya AICC yenye washiriki 11 Bi Zamda Masoud amemshukuru Bwana Mafuru kwa kuiwezesha timu hiyo ushiriki kikamilifu katika michezo hiyo.

Michezo ya SHIMUTA hufanyika kila mwaka na kuwakutanisha watumishi wa Taasisi za umma na Mashirika binafsi kushiriki katika mashindano ya michezo mbalimbali.
Share To:

Post A Comment: