Serikali imeutaka uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwajibika ipasavyo katika kuwapa motisha na hamasa wafanyakazi wa shirika hilo ili kujihakikishia usalama wa reli kiutendaji na miundombinu kama njia ya kuondoa dosari zilizopo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa leo (Oktoba 7,2023) alipofanya mkutano na wafanyakazi TRC katika Stesheni ya Tabora.


Prof. Mbarawa amesema kuwa matatizo mengi yanayolikabili shirika hilo yanatokana na wafanyakazi wengi kukosa hamasa na kuwa na mtazamo hasi jambo linalowafanya kuona reli siyo mali yao bali ni mali ya serikali.

"Lazima tujue hii reli ni yetu na maisha yetu yanategemea ufanisi wake hivyo tunapaswa tuimiliki, tukiweka hilo kwenye ufahamu wetu ninao uhakika kwamba tutaenda vizuri," 
Amesema Waziri Mbarawa.

Pia Warizi Mbarawa ameutaka uongozi kuhakikisha wanawasimamia vizuri wafanyakazi kwani changamoto zilizopo ziko ndani ya uwezo wao na wala haimuhitaji yeye kama waziri ili kuzitatua.


Aidha wakizungumza katika mkutano huo baadhi ya wafanyakazi wamebainisha changomoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa wafanyakazi, ajari za mara kwa mara, kutolipwa kwa malipo ya muda wa ziada pamoja na kutofautiana kwa viwango vya mishahara.

Amina Lumuli ni Afisa Rasilimali Watu TRC, akijibu baadhi ya changamoto amefafanua kuwa changamoto za utofauti wa mishahara kwa baadhi ya kada yanafanyiwa kazi na wamekwisha andika barua kwa afisa utumishi ili kuomba kibali cha kufanya marekebisho hayo.

Hata hivyo Amina amebainisha kuwa tatizo kubwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo ni uadilifu kwani kumekuwa na matatizo mbalimbali yanatotokana na kukosekana kwa uadilifu jambo linaloisababishia serikali hasara kubwa.
"Mara kwa mara tumekuwa tukikamata madumu ya mafuta ambayo wafanyakazi wamehusika katika wizi huo,ilifikia mahali kuna mtu alinyonya mafuta kwenye injini alafu akajaza maji na kusababisha hasara ya bilioni saba," Amefafanua Amina.

Waziri Mbarawa anaendelea na ziara katika shirika hilo ambapo kesho anatarajia kuzungumza na wafanyakazi wa shirika hilo wilayani Katavi mkoani Mpanda na badaye kutembelea mkoani Kigoma huku akibainisha kuwa lengo la ziara hiyo ni kuongeza ufanisi wa shirika hilo la reli nchini.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: