NAIBU Waziri,  Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Adolf Ndunguru kuunda timu ya wataalamu kukagua miradi ya afya na elimu iliyochelewa kukamilika katika Mkoa wa Rukwa na watakaobainika kuchelewesha miradi hiyo wachukuliwe hatua mara moja.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara ya  Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo katika Mkoa wa Rukwa uliofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

 "Katika sekta ya afya Mkoa huu ulipokea fedha zaidi ya Sh. Bilioni 8 kwa ajili ya maboresho ya zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya lakini kwenye ziara yako Mhe.Katibu Mkuu kuna maeneo umepita na kukuta fedha zimekwenda ila majengo hayajakamilika na kuna maeneo umekuta fedha zimekwisha na majengo hayajakamilika na wengine fedha wanazo lakini ujenzi umesimama."

"Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Mohamed Mchengerwa namuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha anaunda timu mara moja itakayokuja Rukwa kufanya uchunguzi wa fedha zote zilizoletwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuboresha afya za wananchi wa Rukwa na fedha hizo zikachezewa na watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao," amesema Mhe.Ndejembi.

Amemhakikishia Katibu Mkuu wa CCM kuwa ndani ya siku saba timu hiyo itakuwa imefika kwa ajili ya uchunguzi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ili kuona ni kiasi gani cha fedha kimetumika na kwanini miradi hiyo haijakamilika na pale itakapobainika kutokea kwa ubadhirifu wa fedha za umma hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Pia ameelekeza timu hiyo kukagua miradi ya elimu kwa shule ambazo zilipelekewa Sh. Milioni 470 kuona ni namna gani zimekamilika na zile ambazo hazijakamilika kuona sababu iliyopelekea kuchelewa kwa miradi hiyo huku akimuahidi Katibu Mkuu wa CCM kuwa hakuna mtu yeyote atakayebaki salama endapo atabainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha hizo za miradi.

Share To:

Post A Comment: