Wataalamu wa Wanyamapori na Maliasili katika nchi za Afrika wametakiwa kuchukua hatua madhubuti za ulinzi wa mnyama aina ya kakakuona ambao wako hatarini kutoweka.

Kakakuona ambae anashika nafasi ya kwanza katika orodha ya mamalia wanaosafirishwa kwa magendo duniani, mbali na kutumika kama nyama adimu nchi za Asia, magamba yake hutumia kutengeneza dawa za jadi zinazotajwa kutibu magonjwa ya pumu na saratani nchini China.

Akizungumza jijini Arusha, mkurugenzi wa kikosi kazi cha makubaliano ya Lusaka (LATF) Edward Phiri alisema kwa sasa ‘kakakuona’ ndio aina ya wanyamapori wanaotafutwa zaidi na wafanyabiashara haramu kwa ajili ya kusafirisha kinyume cha sheria na kuwapeleka katika bara la Asia hivyo kuwaweka katika hatari ya kutoweka katika nchi za Afrika.

Phiri alisema hayo kwenye Mafunzo ya Kikanda ya Kupunguza Usafirishaji wa Wanyamapori Baharini kati ya Afrika na Asia yaliyoaandaa kwa kushirikiana na Taasisi ya Grace Farms Foundation – Marekani kwa maafisa wanyamapori kutoka Kenya, Tanzania na Cambodia

"Kakakuona tayari wametoweka katika bara la Asia na sasa wafanyabiashara wa wanyamapori wameanza kusafirisha viumbe hao kutoka Afrika na kuwapeleka huko ambako wanauawa, kwa matumizi ya kitoweo au dawa za asili ," alisema Edward Phiri.

Phiri alisema jitihada za makusudi zinahitaji katika kuokoa kizazi hicho lakini pia wanyama wengine ambao bidhaa zao zimekuwa lulu kimataifa huku vikwazo vya kimipaka vikishindwa kukamaliza tatizo.

“Mafunzo haya yanalenga kuwasaidia maafisa wetu wa mali asili na wanyama pori kutambua mbinu za kidigitali ambazo wahalifu kwa sasa wanatumia lakini pia kuwafunza umuhimu wa ushirikiano katika kushughulikia kesi hizi ili zilete matokeo chanya katika usafirishaji wa wanyama mipakani”

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Luka Kitandula alisema kuwa  ipo haja kuimarisha uwezo  na kukuza ushirikiano kati ya vyombo vya utekelezaji  wa sheria katika swala la ujuzi kupitia kuongeza ufuatiliaji na kushirikiana kwa taarifa mbali mbali za uhalifu huu.

“uhalifu wa wanyama pori unazidi kuwa wa kisasa na wa kibunifu hivyo ujunzi huu  ni muhimu kutokana na viwango vya sasa vya uhalifu wa wanyama pori katika bara letu na kuhatarisha wanyama husika kutoweka akiwemo ‘Kakakuona’” alisema.

Share To:

Post A Comment: