Na Shaban Juma, Rukwa

Mkuu wa wilaya ya Kalambo Lazaro Komba amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la utoaji wa chanjo kwa watoto chini ya miaka 8 ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Polio.

Kauli hiyo ameitoa leo akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Nyerere wakati wa uzinduzi wa kikao cha kamati ya afya mkoa juu ya uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.

Aidha Mhe. Komba amesema kuwa kila mtoto mkoani Rukwa anapaswa kupata chanjo ya polio kwani itaongeza kinga mwilini na kumuepushia mtoto ulemavu wa kudumu au hata kifo kwani ugonjwa huo hauna tiba.

Sambamba na hilo, Mhe. Komba amesisitiza kwa wazazi kuwapa watoto haki zao za kuwa na afya njema na kuacha mila potofu kwani kufanya hivyo kutaleta madhara makubwa katika jamii.

Hata hivyo, Mhe. Komba amebainisha kuwa malengo ya Mkoa wa Rukwa ni kuwafikia watoto 391,883 kwa kuwapatia chanjo aina ya pili ya polio katika vituo vya Afya na nyumba kwa nyumba.

Mhe. Komba amewataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vya ugonjwa wa polio katika kituo cha afya iwapo dalili za mtu mwenye viashiria vya polio ikionekana ili iwe rahisi kuudhibiti.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: