Tanzania imejipanga kuendelea kushirikiana na wadau kutoka nchi mbalimbali duniani katika kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii nchini.
Hayo yamesemwa leo Septemba 27,2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) mara baada ya hafla ya Ufunguzi ya Siku ya Utalii Duniani iliyofanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia.
“Nimekutana na wenzetu wa Sekta ya Utalii kutoka nchi mbalimbali kama Israel, Indonesia, Miamar, Honduras, Senegal, Sierra Leon pamoja na Mawaziri wengine 45 kutoka nchi hizo ambapo tunaamini huu ni mwanzo mzuri kuhakikisha kwamba tunaendelea kuitangaza nchi yetu ili tuweze kupiga hatua kubwa Zaidi.” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amefafanua kuwa kupitia Mawaziri wa Utalii wa nchi nyingine walioshiriki maadhimisho hayo Tanzania ina mpango wa kukiunganisha Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vingine vya nchi nyingine vilivyopo nje ya nchi ili viweze kushirikiana katika utoaji wa mafunzo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa ni muafaka kulingana na huduma za kitalii ambazo watalii wanazihitaji.
“Tumefurahi kuona hapa Saudi Arabia leo hii wamezindua chuo cha mafunzo ya ukarimu na utalii na sisi Tanzania tumeonyesha nia ya kushirikiana nao katika mafunzo, tutakuwa na mazungumzo na Waziri wa Utalii wa hapa Saudi Arabia kuona ni namna gani Watanzania wanaweza kunufaika.” Mhe. Kairuki amesema.
Aidha, amesema amepata nafasi ya kukutana na wawekezaji mbalimbali ikiwemo wamiliki wa mahoteli ikizingatiwa kwamba Tanzania inatakiwa kuongeza idadi ya vyumba vya kulala kwa ajili ya watalii ambao idadi yao inaendelea kuongezeka.
Amesema Tanzania imepata ujuzi wa namna ya kutumia teknolojia katika kuboresha huduma mbalimbali katika Sekta ya utalii, masuala ya umuhimu wa rasilimaliwatu, ubunifu, kuwekeza katika upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya wafanyabiashara wanaotekeleza miradi mbalimbali ya utalii na kuona ni kwa namna gani nchi zinaweza kuweka mazingira bora kisera,mifumo ya udhibiti, katika masuala ya kisheria pamoja na taratibu nyingine za utoaji wa huduma hasa kwa wateja.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi amesema kuwa Serikali kupitia inatekeleza kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Tourism and Green Investments” yaani Utalii na uwekezaji unaojali mazingira kwa kuwafanya wawekezaji wafuate taratibu wanapowekeza katika hifadhi ili kuhakikisha wanatunza mazingira na kuzingatia jamii inayozunguka eneo hilo.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mawaziri na wawakilishi kutoka jamii za Kimataifa, Serikali, Mashirika ya Fedha, Washirika wa Maendeleo na Wawekezaji kutoka Sekta Binafsi.
Post A Comment: