Na WAF – Dodoma


Waajiri katika sekta mbalimbali nchini wametakiwa kuweka mazingira wezeshi yatakayowasaidia akina mama kunyonyesha Watoto wao wakiwa katika maeneo yao ya kazi.


Wito huo umetolewa leo Agosti 9, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala-Wizara ya Afya Bw. Issa Ngi’mba wakati akifungua kikao cha waajiri kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi chenye lengo la kujadili namna bora ya kuweka mazingira wezeshi ya unyonyeshaji.


Mkurugenzi huyo amesema ili wanawake waweze kunyonyesha vizuri na kwa wakati Watoto wao ni vyema kukatengwa vyumba maalum mahala pa kazi ili mtoto atakapoletwa mama awe na uhuru wa kumnyonyesha mwanae bila kuwa na hofu au mwingiliano wa watu wengine.


“Unyonyeshaji wa mtoto toka anapozaliwa hadi anapofikisha siku elfu moja ni muhimu katika ukuaji wake, na katika kipindi hiki anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee ili aweze kukua na kujenga mwili wake ikiwemo kinga dhidi ya magonjwa hivyo basi kwa akina mama wanaofanya kazi ni muhimu waajiri wao wakatenga maeneo maalum ya unyonyeshaji”. Amesema Bw. Issa.


Aidha, Issa ameongeza kuwa maendeleo ya mtoto yanategemea ukaribu na mama yake ambaye anamnyonyesha kwani maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu ambavyo mtoto anahitaji na anatakiwa kunyonya muda wote na sio kupangiwa ratiba.


Amesema kuwa Wizara Afya kwa kushirikiana na wadau pamoja na taasisi mbalimmbali wana jukumu la kuendelea kutoa elimu kwa waajiri wa sekta rasmi na zisizo rasmi kutenga maeneo hayo ikiwemo sehemu ya Watoto kucheza na kupumzika mara baada ya kunyonya.Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Wizara ya Afya Bi. Neema Joshua amesema kaulimbiu ya mwaka huu imelenga kuona namna gani waajiri wanaweza kuweka mazingira wezeshi ya kuwawezesha akinamama kunyonyesha Watoto wao akiwa kazini.


Kikao hiki cha Waajiri ni mwendelezo wa Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo mwaka huu imebeba kaulimbiu isemayo Saidia Unyonyeshaji: Wezesha Wazazi Kulea Watoto na Kufanya Kazi Zao Kila Siku.
Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: