Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza masikitiko kwa hujuma inayofanywa na madereva wa Serikali dhidi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza jana jijini Dodoma wakati akikabidhi magari 17 kwa Idara ya Kazi (Ofisi ya Waziri Mkuu) na 13 kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mhe. Majaliwa ameagiza kufanyika kwa ufuatiliaji na hatua kuchukuliwa dhidi ya maedereva watakaobainika kujihusisha na hujuma.


“Maafisa Masuhuli na Vyombo vya Usalama wahakikishe wanafanya ufuatiliaji kikamilifu na kuchukua hatua kuhusu taarifa za baadhi ya madereva kujihusisha na wizi wa mafuta kwa kudanganya taarifa za umbali au kuuza mafuta kupitia vituo vya mafuta au kutoka katika magari yao. Vitendo hivi ni ukiukwaji wa masharti ya ajira na hujuma kwa Serikali,” ameagiza Waziri Mkuu.


Pamoja na hilo, Mhe. Majaliwa amewataka madereva wa Serikali kufuata sheria za usalama barabarani na kutojiona kwamba wapo juu ya sheria hizo.


“Kuendesha gari ya Serikali haimaanishi mmepewa rungu la kuvunja sheria bali mnapaswa kuwa mfano wa kuzingatia sheria za nchi kuhusu usalama barabarani,” ameelekeza Waziri Mkuu.


Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Joyce Ndalichako amesema magari hayo 20 na vifaa vya kulinda afya pahala pa kazi vilivyokabidhiwa leo vimegharimu shilingi bilioni 4.3.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: