Na Okuly Julius-Dodoma

KATIKA kukabilia na ongezeko la ajali za barabarani nchini Chuo cha Udereva cha WIDE kwa kushirikiana na Serikali ya wilaya ya Chamwino wameanzisha programu ya mafunzo maalum kwa madereva pikipiki zaidi ya 600.


Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Chuo hicho Faustine Matina, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia elimu bodaboda ambao wamekuwa wakisababisha ajali kutokana na kukosa uelewa wa sheria za usalama barabarani.


“Lengo la mafunzo haya ni kutokana na ongezeko la ajali barabarani na bodaboda ni moja kati ya vyombo ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali kwa wingi hali ambayo inasababisha wengi wao kupata ulemavu na wakati mwingine ajali hizo kusababisha vifo”amesisitiza Matina


Aidha amesema kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali (CAG) ya hivi karibuni inaonyesha kuwa kumekuwa matukio mengi ya ajali nchini ambayo yanasababishwa na waendesha pikikipi maarufu kama bodaboda.


“Matukio hayo mengi yamekuwa yakisababisha vifo na ulemavu kwa baadhi yao hivyo sisi kama chuo kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya Chamwino tumeamua kuunga jitihada zinazofanywa na serikali yetu ya awamu sita kwa kutoa mafunzo haya ambapo yanalenga kuwafikia bodaboda zaidi ya 600 katika kata mbili za Buigiri na Chamwino Ikulu”amesema


Kadhalika, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwafikia waendesha pikipiki wote zaidi ya 1,800 wa wilaya ya Chamwino ili kupunguza ajali za barabarani na kuufanya usafiri huo kuwa salama kwa watumiaji.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buigiri Kenneth Yindi ambaye ndio mhanasishaji Mkuu wa Mafunzo hayo amesema kuwa wanatekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya ya Chamwino la kuwataka Madereva wote wa Bodaboda kupata Mafunzo na leseni ili wawe kamili barabarani na kuepusha ajali.


"Tupo hapa kutekeleza agizo la Mkuu wetu wa Wilaya ambalo ni kuwataka Bodaboda wote kupata Mafunzo haya baada ya hapa hutaruhusiwa kuendesha pikipiki kama huna cheti na leseni ni bora ukafanye kazi nyingine tofauti na Bodaboda,"


Na kuongeza kuwa "hakuna Afisa usafirishaji ambaye Hana cheti Wala leseni ya Udereva Kwa hivyo ili kukidhi vigezo vya kuwa Afisa usafirishaji ni muhimu sana kupata Mafunzo na ukizingatia Chamwino ni Sebule ya Ikulu hatutaweza kuvumilia yeyote ambaye hatakuwa amekamilisha vigezo vya kuwa barabarani,"amesisitiza Yindi


Naye Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Chamwino, ASP Bwire Machunde amewataka waendesha pikipiki wote wa wilaya hiyo kujitokeza kupata mafunzo hayo ili kujengewa uwezo wa kutambua sheria za usalama barabarani na kutambua haki zao.


“Bodaboda wote mnatakiwa kuja kupata mafunzo haya ili kusaidia kupunguza tatizo la ajali nchini mara baada ya mafunzo hayo kutakuwa na msako kwa watu ambao wanaendesha vyombo vyao bila kuwa na mafunzo ya usalama barabarani”amesema ASP Bwire


Baadhi ya bodaboda walioshiriki mafunzo hayo waliishukuru serikali kwa kuwapatia fursa hiyo ambayo inakwenda kuwasadia kuondokana na ajali za barabarini.


Nyemo Chedego, amesema moja ya sababu ambazo zimekuwa zikichangia ongezeko la ajali nchini ni pamoja na bodaboda wengi kuendesha vyombo vya moto bila ya kuwa na mafunzo rasmi kutoka vyuo vinayotambulika.


“Mafunzo haya kwetu yamekuja wakati mwafaka kwani watu wengi wamekuwa wakipata ajali na wengine kufa kutokana na kutokujua sheria za usalama barabarani hivyo mafunzo haya yatakwenda kuwa msaada kwetu kuondokana na hali hiyo”amesema Chedego


Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: