Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kupitia Umoja wa Wakandarasi wazawa Tanzania (ACCT) kimepongezwa kwa jitihada za kuendesha kituo cha mafunzo ya vitendo kwa mafundi mchundo wa fani mbalimbali za ujenzi chenye lengo la kurasimisha ujuzi wao ili uweze kutambulika kwenye soko la ajira
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) alipotembelea Chuo hicho na kufanya ziara kwenye kituo hicho. Prof. Mkenda amesema kwamba kinachofanyika hapo ndio ndoto ya serikali ya kukuza ujuzi kwa vitendo.
“Kinachofanyika hapa ndio ndoto ya serikali na hata ukikumbuka ahadi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alisema tutaimarisha ubora wa elimu yetu na kuongeza ujuzi wa wahitimu katika taasisi zetu za elimu, kinachofanyika hapa ni kujenga mahusiano makubwa Zaidi kati ya kinachofundishwa humu na kinachohitajika sokoni” alisema Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda ameahidi serikali itarudisha mahusiano yaliyokuwepo baina ya kituo hicho na Wakufunzi wastaafu kutoka Uholanzi (PUM) ili waendelee kuleta wakufunzi wao kwenye kituo hicho na pia wakufunzi wetu wa ndani wapate fursa ya kwenda kuona kinachofanyika Uholanzi.
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja huo wa Wakandarasi wazawa Tanzania Mhandisi Milton Nyerere pamoja na Eng Ommary Kiurei ameeleza kuwa lengo la kituo hicho ilikua ni kuongeza uwezo wa ndani wa Wakandarasi wazawa.
“Lengo la kituo hiki ni kuongeza uwezo wa wakandarasi wazawa na kuondoa ile dhana kuwa wandarasi wazalendo wanafanya kazi mbaya, sasa tumeboresha uwezo wetu kwa kuongeza ujuzi kwa mafundi wetu ili tukienda kwenye ushindani wa soko tatizo la ubovu wa kazi tuwe tumeliondoa” alieleza Mhandisi Nyerere.
Kituo cha Mafunzo cha Umoja wa Wakandarasi wazawa Tanzania kilianzishwa mwaka 2015 na kipindi chote kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi ya ujenzi kwenye fani za upigaji plasta, uwekaji wa marumaru, kupaka rangi pamoja na kupamba kuta.
Kwa upande wake aliyekua mkuu wa chuo hicho Dkt Richard Masika ambae pia ni mdau kutoka sekta binafsi amesema kituo hicho kinaendeshwa kwa kushirikiana na umoja wa wakandarasi wazawa nchini na wataalamu wake wanatoka Nethalands katika shirika la Pumu wataalamu wastaafu ambao wamejitolea kutoka ujuzi hapo chuoni .
Post A Comment: