Mtafiti wa Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara, Zamira Matumbo (katikati) akiwaelekeza wanafunzi wa Sekondari ya Ngongo namna bora ya kilimo cha mbogamboga walipotembelea Shamba la taasisi hiyo katika Maonesho ya NaneNane ynayoendelea viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

.......................................................................................................

Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Lindi

TEKNOLOJIA ya mbegu bora ya zao la ufuta inayofundishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara imesaidia kupatikana kwa zaidi ya Sh.Bilioni 160 katika Mkoa wa Lindi na Mtwara baada ya kuuza ufuta katika kipindi cha msimu wa kilimo wa mwaka 2022/ 2023.

Hayo yameelezwa na Mtafiti wa Programu ya zao la Ufuta na Mgunduzi wa mbegu ya ufuta kutoka TARI, Naliendele Mkoa wa Mtwara,  Zabron Ngamba wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya NaneNane 2023 yanayoendelea Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

"Zao la ufuta ni la kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Kusini  na ndio maana sisi TARI tumeendelea kuongeza nguvu zaidi za utafiti wa mbegu bora kwa ajili ya kuliinua kwani soko lake ni kubwa ndani na nje ya nchi," alisema Ngamba.

Alisema kutokana na teknolojia za mbegu bora na ufundishaji wa kanuni za kilimo bora cha ufuta katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 mikoa ya Lindi na Mtwara ilipata zaidi ya Sh.Bilioni 160 kutokana na kuuza ufuta jambo ambalo linaonesha mafanikio makubwa ya kilimo cha zao hilo.

Ngamba alisema mkulima akifuata taratibu na kanuni za kilimo cha ufuta ile tija ya kupata tani moja ya ufuta katika ekari mbili na nusu itapatikana hasa ikitumika mbegu aina ya Lindi 02 mkulima anaweza kupata hata tani moja na nusu.

Ngamba anapenda kuwatoa hofu watanzania na wakulima wa zao hilo na kuwa duniani linahitajika kwa wingi hivyo ni fursa kubwa kuzalisha zao la ufuta kwa wingi na kulipekeka katika soko hilo ambalo hata bei zake zinalizisha na kuwa mkulima wa anauhakika wa kupata faida na sio hasara iwapo tu atazingatia kanuni za kilimo bora cha ufuta.

Aidha Ngamba alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali wakiwemo wa vyama vya msingi na wasimamizi wa vyama hivyo kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora na hata ikiwezekana kuwakopesha mbegu hizo na wakisha zalisha watapeleka mazao hayo kwenye vyama hivyo na kupata faida kwa pande zote na taifa kwa ujumla.

Ngamba aliishuru Serikali kwa kuendelea kuwasapoti watafiti wazao hilo na mazao mengine ambapo alitoa ushauri kwa Serikali katika kila zao linalouzwa nje ya nchi basi kiasi cha fedha zitakazopatikana asilimia 10 itengwe kwa ajili ya kufanya utafiti jambo litakalosaidia kuinua kilimo nchini.

Mtafiti wa Mazao ya Muhogo na Viazi kutoka TARI Naliendele, Festo Masisila akiongelea kilimo cha viazi vitamu na umuhimu wake alisema TARI kupitia vituo vyake vingine tayari vimesajili mbegu za viazi vitamu 16 na ndani ya mbegu hizo kuna mbegu zenye virutubisho vyenye vitamini A aina nane maarufu kama viazi lishe.

Alisema virutubisho hivyo vya vitamini A vinavyotokana na viazi hivyo vinatofautiana kutokana na baina ya mbegu na kuwa zinavumilia magonjwa na zinatumia muda mfupi kwa siku 120 tu tayari zinapelekwa sokoni.

Alisema matumizi ya viazi hivyo vyenye virutubisho vya vitamini A vinapotumika kwa wingi vinasaidia kukabiliana na utapiamlo na uono havifu na hasa kwa watu ambao wapo katika makundi maalum kama watoto wa miaka 0 hadi miaka mitano, wazee pamoja na waathirika wa virusi vya HIV na wanapovitumia mbali ya kuongeza virutubisho hivyo pia wanaongeza nguvu kutokana na kuwa na wanga.

Alisema chakula hicho kinaweza kutumika kama kitafunwa cha chai, chakula cha kawaida ambacho kitasindikizwa na maziwa yaliyogandushwa ‘mtindi’.

Alisema kutokana na umuhimu wa viazi hivyo TARI wamekwenda mbali zaidi na kuviongeza thamani kwa kutengeneza juisi ambayo inaweza kutumiwa na mtu yeyote wakiwemo watoto na kuwa wapo tayari kuwasidia wadau na wajasiriamali kwenda kujifunza teknolojia ya kilimo hicho na namna ya kuongeza thamani ya viazi hivyo.

Alisema soko la viazi hivyo ni kubwa mno akitolea mfano mtu akivipekeka sokoni na akawakuta wenzake wanavyo vile vya asili itabidi wasubiri kwa muda kuuza vya kwao mpaka huyo mwenye viazi lishe avimalize na hiyo inatokana na wateja kuvigombania.

Masisila aliwaomba wananchi na wakulima kufika banda la TARI lililopo kwenye viwanja hivyo vya NaneNane Ngongo kwenda kujifunza teknolojia ya kilimo hicho na namna ya kupata mbegu bora.

Masisila alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza kutoka nje virutubisho vya vitamini A, kuwagharamia wataalam na wasambazaji  ambapo ametowa wito kwa wadau na makundi mengine kujikita katika kuongeza uzalishaji wa viazi hivyo jambo litakalosaidia kupunguza matumizi ya manone ya vitamini A kutoka nje yanchi kikubwa ni kuongeza nguvu kwa kuwawezesha wakulima waweze kuzalisha kwa wingi viazi hivyo.

Mtafiti Mwandamizi Benadetha Kimata kutoka TARI Naliendele ambaye ni mbobezi wa zao la Muhogo alisema zao hilo ni la muhimu sana katika mikoa ya Kanda ya Kusini na kuwa asilimia 28 ya muhogo unaozalishwa hapa nchini unatoka katika kanda hiyo.

Alisema zipo aina ya mbegu mbalimbali kuna zile ambazo zinachangamoto ya magonjwa na wadudu akitolea mfano wa zile za asili kama Albert au Mleteta ni mbegu ambazo zinaugua ugonjwa wa mchirizi kahawia na magonjwa ya batobato ambayo yana hasara kubwa kwa mkulima asilimia 50 hadi 100 kwa ugonjwa wa batobato na hasara yaasilimia 75 hadi 85 kwa ugonjwa wa michirizi ya kahawia.

Kimata alisema kutokana na mazao hayo ya mbegu za asili kuwa na ukinzani mdogo wa magonjwa na uwezo wa kuzaa kuwa na tija ndogo kiasi cha wastani wa tani 8 kwa hekta mbili na nusu ukilinganisha na mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na TARI zenye tija kubwa kiasi cha tani 20 kwa wastani hadi tani 50 kwa hekta mbili na nusu ambapo wanawashauri wakulima kutumia mbegu hizo.

Alisema mkulima akitumia mbegu hizo bora anakuwa na nafasi nzuri ya kuwa na chakula cha kutosha katika kaya yake, jirani na katika nchi na kupata kipato kutokana na mauzo ya muhogo na bidhaa zake.

Alitaja bidhaa za muhogo kuwa ni unga, wanga na kutokana na unga mkulima anaweza kutengeneza vyakula mbalimbali kwa kutumia unga huo kama ilivyo ngano kutokana na ngano ilinayozalishwa nchini kutotosheleza mahitaji ya watumiaji hadi kufikia hatua ya kuagizwa kutoka nje.

Kimata alisema wanapohimiza na kuhamasisha uzianzishwaji wa viwanda vya kusindika muhogo wana lenga kuipunguzia Selikali ya kuagiza ngano kutoka nje na watu wakatumia muhogo ambao unazalishwa nchini kwa kutengeneza mkate, maandazi na vyakula vingine vinavyofanana na bidhaa hizo za kuoka.

Alisema jambo hilo aliwezi kufanyika bila ya kuwepo Sera ya Kiserikali ambayo itasaidia kuwahimiza wanao pika mikate na mazao mengine madogo madogo yanayo okwa kuweka walau hata asimilia moja hadi tano ya unga wanao hutumia kuzalisha bidhaa hizo wakatumia unga wa muhogo na kuwa hilo ndilo ombi lao kwa Serikali.

Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano wa TARI Naliendele akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dk. Fortunus Kapinga aliwaomba wananchi wa mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara kufika kwenye banda lao kujifunza teknolojia za kilimo kwani wapo watafiti wabobezi wa mazao yanayosimamiwa na kituo hicho. 

Mtafiti wa Programu ya zao la Ufuta na Mgunduzi wa mbegu ya ufuta kutoka TARI, Naliendele Mkoa wa Mtwara,  Zabron Ngamba, akizungumzia kilimo cha zao la ufuta.
Mtafiti Mwandamizi Benadetha Kimata kutoka TARI Naliendele ambaye ni mbobezi wa zao la Muhogo akizungumzia kuhusu kilimo cha zao hilo.
Mtafiti Msaidizi wa Kilimo kutoka TARI Naliendele,  Dickson Malulu, akielezea kilimo cha mbogamboga ambapo anawahamasisha vijana kujikita katika kilimo hicho cha muda mfupi ambacho kitawaingizia fedha kwa haraka badala ya kusumbilia kilimo cha korosho ambacho kinachukua muda mrefu kupata fedha.
Mtafiti wa Kilimo wa mazao ya Nafaka na Mikunde, Dk. John Tenga, akizungumzia kuhusu kilimo cha mazao hayo.
Muonekano wa mboga aina ya Chinese zilizopo katika shamba darasa katika maonesho hayo.
Wadau waliotembelea banda la TARI kwenye maonesho hayo wakipatiwa maelekezo ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo na Afisa Kilimo wa TARI Naliendele, Rozalia Simchimba (kushoto).
Muonekano wa shamba darasa la zao la ufuta kwenye maonesho hayo.
Muonekano wa Shamba la Alizeti kwenye shamba la TARI Naliendele.
Afisa Kilimo Sara Mkuchu kutoka TARI Naliendele akimuelekeza jambo mkulima aliyetembelea shamba la mtama la taasisi hiyo.
Muonekano washamba la muhogo la TARI Naliendele.
Vijana wakichagua mbogamboga katika shamba la mfano katika maonesho hayo.
Muonekano wa shamba la ndizi aina ya Mtwike kwenye maonesho hayo.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: