Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde anatarajia kuandaa mafunzo maalum kwa walimu wa Sayansi na Mafundi sanifu wa Maabara za Shule za sekondari Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo na maarifa zaidi katika matumizi ya vifaa vya maabara.

Mavunde kayasema hayo jana katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge iliyopo Kikombo,Dodoma Jiji wakati akikabidhi seti ya Televisheni na King’amuzi cha kwa ajili ya matumizi ya Shule ikiwa ni utekelezaji wake wa ahadi aliyoitoa wakati wa mahafali ya Pili ya Kidato cha Sita shuleni hapo.

“ Tunawashukuru wabunge kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta ya Elimu uliowezeshwa kujengwa kwa Shule hii ya wasichana ya mchepuo wa Sayansi.

Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya zaidi ya bilioni 2 katika kuiboresha shule hii.

Ninawakabidhi TV hii ambayo ni “_smart TV_” kwa lengo la kuwasaidia kupata habari mbalimbali na kujifunza zaidi katika eneo hili la sayansi,na pia nawashukuru Kampuni ya Multichoice Tanzania kwa kutoa king’amuzi bure na kuwalipia miezi mitatu ya mwanzo.

Tutahakikisha tunatumia mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaopita hapa Dodoma kuongeza ufanisi wa masomo ya sayansi kupitia Teknolojia.

Ofisi ya Mbunge itaandaa mafunzo maalum kwa walimu wetu wa sayansi na mafundi sanifu wa maabara ili kuwaongezea maarifa katika matumizi ya vifaa vya maabara ambayo mwisho wa siku yataleta tija kwa maendeleo ya wanafunzi”Alisema Mavunde

Wakishukuru kwa pamoja Diwani wa Kata ya Kikombo Mh. Emmanuel Manyono na Diwani Viti Maalum Mh. Wendo Kutusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Ndg. Fred Mushi wamemshukuru Mbunge kwa kuwajali wanafunzi na kutimiza ahadi yake kwa Shule ya Sekondari Bunge.

Akitoa taarifa ya awali,Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunge Mwl. Salome Mkombola amesema kwamba wamejipanga vizuri kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kwenye taaluma kwa kuzalisha wanasayansi wengi wa kike wenye uadilifu na nidhamu kubwa.

Share To:

Post A Comment: