Na. Majid Abdulkarim, Mbarali


Wagonjwa zaidi ya 500 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanatarajiwa kupatiwa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kutoka kwa madaktari bingwa wa macho ambao wameweka kambi ya wiki moja katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Kanali Dennis Mwila wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho itakayodumu kwa muda wa siku saba Wilayani hapo.

Kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu, ambapo wakazi wa Wilaya hiyo wanaendelea kupata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Kanali Mwila amesema kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia Moja ya watu wanapata matatizo ya macho.

Aidha, Kanali Mwila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Helen Killer kwa kuanza kampeni ya kutokomeza magonjwa ya macho Juni 2022 ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya Sh: Mil. 140 kwa Mkoa wa Mbeya na walitoa mafunzo kwa watumishi wa Afya ngazi ya jamii wapatao 570.

“Juni, 2022 Shirika la Helen Killer liliweza kugundua wagonjwa 1,750 ambao walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho kwa awamu tatu tofauti”, ameeleza Kanali Mwila.

Amesema, katika kambi hiyo inayoendelea jumla ya watu 500 wanatarajiwa kupatiwa huduma ambapo zaidi ya kiasi cha Sh: Mil. 110 kitatumika katika kuwapatia huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Amesema, kwa mwaka jana (2022) wagonjwa 29,000 waliyo onwa katika Mkoa Mbeya, wagonjwa 3,406 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho na magonjwa mengine.

Vile vile, Kanali Mwila ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa imara katika kuwasogezea huduma za Afya karibu.

Naye, Meneja Mpango wa Taifa wa Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Bernadetha Shilio amesema kuwa mbinu inayotumika kuwapata wagonjwa ni kupitia wahudumu ngazi ya jamii ambao wanaambatana na wataalamu wa Afya nyumba kwa nyumba na kuwabaini wagonjwa.

Dkt. Shilio amesisitiza kuwa Huduma za upasuaji katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali zinatolewa bila malipo chini ya ufadhili wa Shilika la Kimataifa la Helen Killer.  

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mratibu wa Macho kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ernest Paul amesema Serikali itahakikisha inawezesha upatikanaji wa huduma za macho karibu na wananchi hususani ngazi ya msingi.
Share To:

Post A Comment: