.


 NNa, WAF, Dodoma


Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuongeza kasi na Ufanisi wa utoaji elimu kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma bora za afya nchini.

Mhe. Nyongo ameyasema hayo leo Agosti 16, 2023 baada ya kupokea taarifa ya Mfuko wa Bima ya Afya iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Bw. Bernard Konga katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

Aidha, Mhe. Nyongo amesema kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya itapunguza malalamiko kwa wananchi ambao hawakua na uelewa kuhusiana na huduma za Mfuko huo.

“Mkiongeza ufanisi katika utendaji kazi wenu na watu wakapata uelewa wa kutosha itatusaidia sana kwenda kwenye hatua nyingine, wabunge na wananchi wataelewa na kuuamini zaidi mfuko huo”, amesema Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesisitiza kuchukuliwa hatua kwa vituo na wanachama wadanganyifu ili mfuko huo uweze kutoa huduma bora na za  kiuhalali kwa wanachama.

Hata hivyo Mhe. Ummy ameutaka Mfuko huo kuongeza wanachama ili mfuko uweze kukua na kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wa NHIF.

Waziri Ummy amesema wamepokea maoni kutoka kwa wajumbe wa kamati hiyo na kuangalia upya muundo wa Taasisi hiyo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania juu ya magonjwa yasiyoambukiza ili kuupunguzia mzigo NHIF na kuokoa maisha ya wananchi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga amesema, Katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023 mfuko kupitia Kitengo cha Kudhibiti na kupambana na udanganyifu, uliweza kubaini madai yasiyo halali ya shilingi bilioni 7.26 kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.

“Baada ya kubaini madai yasiyo halali ya Tsh: bilioni 7.26 tumefanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kutoka katika vituo husika vilivyofanya udanganyifu huo”, amebainisha Bw. Konga

Aidha, Bw. Konga amesema kuwa wamesitisha mikataba 13 baina ya mfuko na watoa huduma baada ya kubaini udanganyifu hivyo kufanya jumla ya mikataba 48 kusitishwa tangu mwaka 2018


Share To:

Post A Comment: