Na. Damiana Kunambi, Njombe


Zaidi ya sh. Mil. 400 zimetolewa na serikali ili kujenga soko la Samaki la kisasa katika Kata ya Manda Wilayani Ludewa mkoani Njombe ambalo litatumiwa na wavuvi wa ukanda huo katika kufanya biashara na kuhifadhi samaki zao kwakuwa kutakuwa na majokofu ya kisasa.

Hayo ameyasema mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipowasili katika kijiji cha Iwela kata ya Iwela ikiww ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kijiji kwa kijiji kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 6 kati ya 77 vlivyopo wilayani humo.

"Nilijenga hoja bungeni juu ya kuanzishwa kwa hili soko nashukuru hoja yangu imeonekana kuwa na mshiko kwkuwa ni hoja inayoenda kukuza uchumi hivyo namshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha hizi ambazo zinaenda kuleta chachu ya maendeleo katika jimbo hili". Amesema Kamonga.

Ameongeza kuwa kutokana na mpango huo wa uanzishwaji wa soko la samaki aliona ni vyema kuanzisha ufugaji samaki katika vizimba ili soko hilo liweze kusheheni samaki wa kutosha ambapo kupitia mfuko wa jimbo alitoa kiasi cha sh. Mil. 20 .5 ambazo ziliwezesha kuanzisha vizimba vya majaribio ambavyo vimewekwa katika kitongoji cha Chuva katika kijiji hicho na mpaka sasa tayari vimeonekana kuwa na matokeo mazuri.

"Ziwa letu linafaa kwa ufugaji kwani kuna kipindi kulikuwa na upepo mkali, mawimbi na hata kile kimbunga Fred kilifika kidogo huku kwetu kikitokea nchini Malawi lakini kizimba chetu hakikuweza kuathiriwa na chochote hivyo nikaona kumbe ziwa letu linafaa kwa ufugaji na linaweza kutuzalishia samaki wengi". Amesema Kamonga.

Amesema samaki waliowekwa katika kizimba hicho ni aina ya perege ambapo kutokana na wingi wa joto lililopo katika eneo hilo linawawezesha kukua kwa haraka ambapo hukua kwa kipindi cha miezi 4 badala ya miezi 6.

Aidha kwa upande wa wananchi wa kata hiyo wamempongeza mbunge huyo kwani wamekuwa wakifanya uvuvi wa kizamani ambao hauwapi manufaa yoyoye.

Mikael Haule ni mmoja wa wananchi hao amesema wamekuwa wakivua samaki kwa kutumia zana hafifu hivyo kwa mkakati huo utawawezesha kupata samaki kwa wingi na walio wakubwa.


Share To:

Post A Comment: