Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kuboresha mifumo ya umwagiliaji kwa wakulima wa Chato walio pembezoni mwa ziwa Viktoria kwa kuweka Pampu kubwa za kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kwa kuvuta maji kutoka ziwani kwenda kwenye mashamba ya wakulima.
Hayo yamesemwa Jana tarehe 11 Julai, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde katika viwanja vya Bwera Wilayani Chato aliposhiriki zoezi la Uzinduzi wa Kampeni ya Mapinduzi ya Kilimo na Uchumi Wilayani Chato.
"Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekipa kilimo kipaumbele na kuwajali wakulima wa nchi hii, hilo linajidhihirisha kwa ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 miaka miwili iliyopita hadi kufikia bilioni 970".
Ongezeko hilo la bajeti, pamoja na kazi zingine tumezielekeza kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa mabwawa, ujenzi na ukarabati wa skimu na ujenzi wa visima zaidi ya 27,000 nchi nzima. Aidha, katika ujenzi wa visima, yale maeneo yenye uhakika wa maji, tutakwenda kuwapatia Pampu maalumu ili ziwasaidie wakulima kutoa maji kwenye chanzo na kuyapeleka mashambani.
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija na kupata manufaa kutokana na kilimo chao, uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, ruzuku ya mbolea na huduma za ugani ni viashiria vya hamasa na mwelekeo wa Serikali kuhakikisha mapinduzi ya kilimo yanafikiwa na kumnufaisha mkulima" alisema Mhe. Mavunde.
Katika hatua nyingine, Mavunde alionesha kufurahishwa na jinsi Uongozi wa Wilaya walivyojipanga na kuweka mikakati ya kufanya mapinduzi ya kilimo, na kuahidi kwamba Wizara ya kilimo ipo tayari kuja kuanzisha mashamba makubwa kwa ajili ya mradi wa vijana ujulikanao kama Building a Better Tommorow (BBT) ili vijana na wanawake wa Chato wanufaike na mradi BBT.
Akiwa katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mavunde alishuhudia utiaji Saini wa mikataba ya utatu, baina ya vyama vya ushirika, Bodi ya Tumbaku na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na upande wa tatu ni Benki. Mhe. Mavunde alipongeza tukio hilo na kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kutokana na kupatikana kwa soko la uhakika.
Awali, akitoa salamu za wananchi wa Jimbo lake, Mbunge wa Chato Mheshimiwa Dkt. Medard Matogoro Kalemani alishukuru Serikali kwa jinsi inavyoendelea kulikumbuka Jimbo lake katika sekta ya kilimo ikiwemo mpango wa ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ya Nyisanzi na Mwabasabi, ukarabati na ujenzi wa skimu mpya za umwagiliaji ili wakulima wazalishe kwa tija na kuiomba serikali kuweka mifumo ya umwagiliaji katika maeneo ambayo ni rahisi kufanyika shughuli za kilimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mheshimiwa Deusdedith Katwale alieleza kwamba uongozi wa Wilaya upo tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili kuhakikisha Ajenda 10/30 na mapinduzi ya kilimo wilayani Chato yanafikiwa na kutekelezwa kwa ufasaha ili kuongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.
Post A Comment: