HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kupata Hati safi ya ukaguzi kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2022 na kuupa heshima Mkoa wa Dodoma.

Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliposhiriki Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa kupitia na kujadili hoja za halmashauri zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

“Mstahiki Meya naomba nitumie nafasi hii kwa namna ya pekee na kwa idhini yako Mstahiki Meya kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupata Hati safi ya ukaguzi kwa hesabu zinazoishia tarehe 30 Juni, 2022. Hongera sana. Hati hii safi ya ukaguzi inalifanya Jiji la Dodoma kuendelea kupata Hati safi kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2017/2018. Kitendo hiki kimelipa heshima Jiji la Dodoma, kimeupa heshima Mkoa wa Dodoma na taifa kwa ujumla kwa kweli mmetupa heshima wote” alisema Senyamule kwa furaha isiyo kifani.

Akiongelea chachu ya mafanikio ya Jiji la Dodoma katika ukaguzi huo alisema ni ushirikiano uliopo. “Mstahiki Meya, mafanikio haya makubwa yanatokana na uwepo wa ushirikiano chanya baina yenu waheshimiwa madiwani, watendaji wa halmashauri, viongozi na wadau mbalimbali. Hivyo, nawasihi endeleeni kudumisha ushirikiano huo ili kuiwezesha halmashauri kuendelea kupata Hati safi katika kaguzi zote kila mwaka kama ambavyo imekuwa utamaduni wenu. Ni matumaini yangu kuwa mtautumia ushirikiano huu kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mkaguzi wenu wa ndani zinashughulikiwa ipasavyo ili ziweze kuhakikiwa na kufungwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za serikali” alisisitiza Senyamule.

Mwenyekiti wa mkutano huo maalum Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza taasisi kufuata maagizo na kanuzi zinavyoelekeza katika matumizi ya fedha za serikali. “Mheshimiwa Rais akaenda mbali zaidi na kututaka hesabu zetu ziwe waziwazi na masuala ya kiutawala. Hatuna budi kumpongeza. Ukiangalia mwenendo wa hizi hoja bado tunahitaji msisitizo.  Halmashauri ya Jiji la Dodoma hatuna budi kujisifia na kujipongeza, kwamba bajeti ikiongezeka na kufikia hata bilioni 150 na zaidi ungetemea makosa yawepo zaidi na hivyo, hoja kuongezeka… lakini wakati bajeti yetu inakwenda juu, sisi idadi ya hoja inakwenda chini, kwa nini tusijipongeze katika hili” alihoji Prof. Mwamfupe.

Awali akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa wakati taarifa hiyo inatoka halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 54. Alisema kuwa kati ya hoja hizo, hoja 21 zilikuwa za miaka ya nyuma na hoja 33 zilikuwa za mwaka wa fedha 2021/2022.

“Baada ya majibu ya hoja hizo kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na uhakiki kufanyika hoja 21 zilifungwa na kusalia na hoja 33. Katika ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2021/2022 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametoa Hati safi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hati hii inafanya Jiji la Dodoma kuendelea kupata Hati safi toka mwaka 2016/2017 hadi mwaka 2021/2022 mfululizo” alisema Kaunda.

Akiongelea taarifa ya utekelezaji wa maagizo ra Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema kuwa halmashauri ilikuwa na maagizo 10. Maagizo manne yametekelezwa na maagizo sita yanaendelea kutekelezwa. “Pamoja na taarifa hii fupi, nimeambatisha hoja zinazoendelea na utekelezaji, maoni ya Mkaguzi, majibu ya Menejimenti, maoni ya Kamati ya Ukaguzi na maoni ya Kamati ya Fedha na Utawala, kwa ajili ya kuzipokea, kuzijadili na kutoa maoni na mapendekezo” alisema Kaunda.

Mkutano maalum wa Baraza la madiwani utekelezaji wa maelekezo ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu za mwaka 2021/2022 iwasilishwe na kujadiliwa na Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani mara baada ya kupokelewa.


Share To:

Post A Comment: