Na John Walter-Manyara

Kikao cha Halmashauri kuu ya chama Cha Mapinduzi mkoa wa Manyara kilichoketi julai 15,2023 kimewataka Watanzania wasikubali kupotoshwa juu ya makubaliano yaliyofanywa na Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji bandari ya Daressalaam kwa sababu utakuwa na manufaa mengi kwa Taifa.

Wameeleza kuwa mkataba huo utarahisisha shughuli za Bandari ya Dar Salaam kufanyika kwa ufanisi na kuondoa vikwazo vya ucheleweshaji wa mizigo kwa muda mrefu uliokuwa awali.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara Peter Toima wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi za chama hicho mkoa zilizopo mjini Babati ambapo amewataka watanzania wapuuze mijadala inayoendelea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba bandari imeuzwa.

Amesema kuna watu wametengeneza uongo ili kusapoti dhamira ya kupotosha uboreshaji wa bandari nchini.

"Tunamuomba Rais Samia asikatishwe tamaa wala maneno  yanayozungumzwa na baadhi ya watu ambao lengo lao ni kupinga maendeleo ya nchi" alisema Toima 

Ameiomba serikali itekeleze kwa haraka azimio hilo ili manufaa yaweze kuonekana katika bandari na kwamba mkoa wa Manyara upo pamoja naye katika hilo.

Naye kaimu katibu wa CCM mkoa wa Manyara Filbert Mdaki amesema azma ya serikali inayoongozwa na Rais Samia kuingia makubaliano ya ushirikiano kibiashara ni sahihi na kwamba chama kipo nyuma yake kumuunga mkono kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Aidha kikao hicho cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Manyara,  kimempongeza mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Rais Samia  Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza nchi na kuhakikisha amani,umoja na utulivu uliopo unadumu na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uchumi bila wasiwasi.

Akizungumza kuhusu hilo  Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, amesema mkataba huo ni wa CCM sio mtu mmoja akisisitiza kuwa suala hilo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 Ibara ya 59 ukurasa wa 92 kuhusu uboreshaji wa bandari.

Makubaliano ya ngazi za kiserikali yanayohusu uboreshaji na uendeshaji wa bandari nchini Tanzania tayari yameshapingwa mahakamani na wanasheria waliofungua kesi kutaka kujua uhalali wa mkataba huo.

Miongoni mwa wanasheria waliofungua kesi hiyo ni Wakili Boniphace Mwabukusi anayedai kwamba, "mkataba huo ni batili", akiongeza kuwa Watanzania wengi hawakushirikishwa.

Mawakili hao wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeyadhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania kwa kutuhuma za kusaini mkataba huo wa kimataifa na kuupeleka bungeni kwa ajili ya kupitishwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao.

Share To:

Post A Comment: