Dawa za kulevya ni kemikali ambazo zikiingia mwilini, huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia matendo, hisia, fikra, na muonekano tofauti na matarajio ya jamii. Kemikali hizo zinatokana na mimea, pia madini ambayo yana mahitaji mengine kwa mwanadamu, huingia mwilini kwa njia kuu tatu, kunywa au kula, kuvuta, na kujidunga sindano. Zipo dawa za kulevya zilizoruhusiwa kisheria kama vile tumbaku na pombe, na kwa matumizi ya hospitali kuna Valium, Pethedine, Morphine. Pia zisizoruhusiwa ni kama bangi, mirungi, cocaine, heroin na mandrax.

Tatizo la madawa ya kulevya limetokea kuwa janga kubwa duniani kote, watu wengi wameathirika na janga hili. Jinsia zote wanaume, wanawake, vijana, watoto, na wazee pia. Hapa tutaongelea aina mbili za madawa ya kulevya, yaani bangi na mihadarati (mirungi).

Kundi kubwa linalokabiliwa na kasia hii ya usafirishaji na utumiaji wa dawa hizo ni kundi la vijana kuanzia miaka 15 na hii huchochewa na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii inayoonekana kuwa na faida hasi na chanya katika ukuaji wa diplomasia ya uchumi kwa mataifa mbalimbali duniani.

Matumizi ya madawa ya kulevya ni miongoni mwa matukio ya kihalifu yanayovuka mipaka kutokana na biashara hiyo kuwa ya kwanza duniani kote katika nyanja za uvukaji mipaka, usafirishaji wake huusisha magenge makubwa ya kihalifu kwa kushirikiana na makundi ndani na nje ya nchi yaliyokosa uzalendo na uaminifu kwa taifa lake. 

Wakati mwingine, hata maofisa waliopo kwenye taasisi za serikali huvunja kiapo cha utii kwa kujihusisha na biashara hiyo. Watoto na wanawake wamekuwa wakitumika katika kusafirisha madawa hayo, kutokana na wasambazaji wengi kubaini makundi hayo kuwa ni rahisi kutumia kutokana na hali ngumu za kiuchumi zinazowakabili. Hivyo, watoto wengine hurubuniwa na wengine kutokujua madhara ya kufanya kitendo hicho.

Katika mpaka wa Tanzania na Kenya wilayani Longido mkoani Arusha na Kajado nchini Kenya ni miongoni mwa mipaka mikubwa inayoziunganisha nchi hizi, pamoja na mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kwa upande wa usafirishaji na usambazaji wa madawa ya kulevya kupitia mpaka huo, dawa aina ya bangi na mihadarati (mirungi) husafirishwa zaidi.

"Mpaka huo ni mkubwa na una vipenyo vingi sana vya kuingia Tanzania na Kenya, na baadhi ya vipenyo hutumia usafiri wa magari, pikipiki, na miguu. Pamoja na hayo, kuna baadhi ya maeneo nchini yaliyopo pembezoni na nchi ya Kenya hufanyabiashara kwa thamani ya fedha ya nchi hiyo, ikiwemo kijiji cha Wosiwosi kilichopo kata ya GelailumbwaTarafa ya Ketumbeine wilayani Longido."

Hali hii hutokana na taifa la Kenya kuamini na kuhalalisha matumizi ya mihadarati nchini humo, tofauti na nchi pacha Tanzania ambayo ni haramu na kosa la jinai. Bangi huonekana kulimwa maeneo yote ya nchi hizi, na pia nchi hizi zinaamini kuwa bangi ni haramu na kosa la jinai. Hivyo, Kenya na Tanzania kwa pamoja hukemea matumizi ya bangi na biashara yake.

Nchi wanachama wa EAC, pamoja na kukubaliana kuwepo kwa makubaliano ya diplomasia ya uchumi, zilipaswa kuangalia suala la matumizi ya madawa ya kulevya na kuweka makubaliano ya pamoja namna ya kudhibiti na kuondoa uhalali kwa baadhi ya nchi kuidhinisha matumizi ya madawa hayo, pamoja na kuwa Kenya hujipatia kipato kupitia mihadarati.

Nchini Tanzania, serikali kwa kushirikiana na raia wema inajitahidi kupambana, kudhibiti, na kukemea matumizi ya madawa ya kulevya. Tanzania haijashindwa kudhibiti madawa hayo na haitowahi kushindwa, kutokana na raia wa nchi hiyo kuonekana kutii mamlaka na kufichua au kutoa taarifa za usambazaji haramu na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Tatizo kubwa lililopo ni baadhi ya mataifa jirani na Tanzania kuidhinisha matumizi ya dawa za kulevya, kama vile mihadarati. Hivyo, wananchi wengi wa mataifa haya, hususani wale waishio mipakani, asilimia chache huwa waaminifu na wazalendo. Wengi wao wakiwa wajanja-wajanja na wanaojishughulisha na matukio ya kihalifu yanayovuka mipaka, ikiwemo usafirishaji wa madawa ya kulevya. Katika wengi wao, kuna maofisa wa serikali wanaoshirikiana na raia hao kuingiza na kusambaza madawa hayo.

Mpaka wa Namanga, watoto wengi hutoroka shule au kuacha masomo na kutumika kusafirisha mihadarati na bangi. Raia mzalendo anadai kuwa siku moja akiwa maeneo ya Buguruni Namanga upande wa Tanzania, alimuona mtoto mwenye miaka kama 10 akiwa amebeba mfuko ambao ndani yake kulikuwa na sado (galoni la wazi). Kwa maelezo yake, alidai kuendelea kumfuatilia kwa karibu anaelekea wapi.

"Mtoto yule alikuwa akielekea upande wa Kenya, kabla hajaingia Kenya nilimwendea na kumuuliza umebeba nini. Mtoto yule alionyesha hofu, lakini mwisho wa siku nilifungua mfuko ule na kukuta alikuwa amebebeshwa bangi. Nikamuuliza umetoa wapi na unapeleka wapi? Akadai alitumwa na baba yake mzazi apeleke kwa mama mmoja upande wa Kenya. Nilimshika mkono nikamwambia nipeleke hadi nyumbani kwenu. Tulielekea na tulipofika, baada ya baba wa mtoto kutuona, alikimbia na kumuacha mwanaye."

Watoto wanaosoma mpakani Namanga Tanzania wapo hatarini kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Wazazi na walezi wa watoto katika eneo hilo walipaza sauti zao mwaka 2022, siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Afrika, ambapo Mch. Obadi Kiango alishauri nyumba zinazofanya biashara ya bangi ziweze kufungiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wamiliki wa nyumba hizo.

"Ukitafuta vijana waliomaliza kidato cha nne kanisani, hakuna ilitokea fursa. Akapatikana mmoja tu, wengine tulilazimika kuwachukua nje ya eneo hili. Watoto wote wamekimbilia kwenye biashara ya bangi na mihadarati."

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo, akiwa mkoani Mtwara kwenye uwashaji wa Mwenge wa Uhuru 2023, alisema mkakati wao ni kuhakikisha Tanzania inadhibiti kutumia na kuuza madawa ya kulevya nchini. Rai yake kwa wauzaji na wasambazaji ni kuacha biashara hiyo kutokana na ujio wa msako utakaoanza nchi nzima. Huku akiwaomba viongozi wa dini kutumia majukwaa ya mahubiri kuelimisha jamii juu ya athari ya matumizi na usambazaji wa dawa hizo. 

"Walimaji wa bangi na mirungi tutahakikisha tunawakamata na kutokomeza biashara zao. Kikubwa, jamii itoe ushirikiano, kwani madawa ya kulevya hupoteza nguvu kazi ya taifa. Tutakomesha ndani ya nchi na nje ya mipaka yetu," alisema Lyimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Madawa na Uhalifu - UNODC, Ghada Waly, alitoa ripoti iliyoonesha idadi ya watu wanaotumia mihadarati duniani imeongezeka. 

Mwaka 2020 pekee, watu milioni 275 duniani kote walitumia mihadarati, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.

"Zaidi ya watu milioni 36 wamepata shida kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya.Dawa hizi zimesababisha vifo vya takriban watu nusu milioni kwa mwaka 2019."amesema Mkurugenzi huyo mtendaji wa UNODC. 

Vile vile, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022, takribani watu milioni 284 wenye umri wa miaka 15-64 walitumia dawa ulimwenguni kote mnamo 2020, ongezeko la asilimia 26 katika muongo uliopita. 

"Vijana wanatumia dawa nyingi zaidi, na viwango vya matumizileo katika nchi nyingi ni vya juu kuliko kizazi kilichopita."

Barani Afrika na Amerika Kusini, watu walio chini ya umri wa miaka 35 wanawakilisha watu wengi wanaotibiwa matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya. Imeeleza taarifa ya UNODC iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Vienna, Austria.

Ulimwenguni, ripoti hiyo inakadiria kuwa watu milioni 11.2 kote ulimwenguni walikuwa wakijidunga madawa ya kulevya. Karibu nusu ya idadi hii walikuwa wanaishi na ugonjwa wa hepatitis C, milioni 1.4 walikuwa wanaishi na Virusi Vya UKIMWI, VVU, na milioni 1.2 walikuwa wanaishi na magonjwa yote mawili.

Share To:

Post A Comment: