Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima akimkabidhi mmoja wa wakazi wa Mkoa wa Morogoro Mtungi wa gesi kwenye Uzinduzi wa Kampeni ya Mazingira na matumizi ya Nishati safi na salama iliyoandaliwa na kampuni ya Taifa Gas.


 NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

Mpango wa serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaachana na matumizi kuni na mkaa, kuanza wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

Tayari mikakati imeshaanza ya kupunguza matumizi ya Nishati  chafu kwa wakazi wa Morogoro, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adamu Malima amegawa mitungi 300 ya gesi kwa wakazi wa mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa huku kipaombele kikiwa kwa mama lishe na baba lishe ambao wamekuwa wakitumia Nishati hiyo kwa asilimia kubwa.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adamu Malima amesema matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa athari zake ni kubwa kwa binaadamu ikiwemo magonjwa katika mfumo wa upumuaji pamoja na uharibifu wa mazingira.

Aidha anasema, sehemu ya mikakati ya serikali ni  taasisi za elimu kupitia wanafunzi kwenye shule za bweni, jeshini na kwenye makambi mbalimbali kuacha matumia kuni na mkaa badala yake watumie Nishati Safi na Salama.

Kaim Mkurugenzi wa kampuni ya Taifa Gas Bhoke Angel amesema kampeni hiyo inalenga kupunguza ukataji wa miti kiholela kwajili ya mkaa na kuni kwenye misitu asilia pamoja na utunzaji wa mazingira.

Amesema Kampeni hiyo imehusisha mikoa ambayo imeathilika zaidi na ukataji wa miti ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tabora na Tanga na kwamba mitungi elfu 5 ya gesi itatolewa na wakazi wa mikoa hiyo ili waondokane na matumizi ya mkaa na kuni.

Mwakirishi wa Kamanda wa kanda ya Mashariki TFS, Afisa Mhifadhi Mkuu wa misitu Wilaya ya Morogoro Patricia Manonga amesema wao kama TFS wataendelea kulinda na kuhifadhi misitu asalia ambayo imekuwa ikiathiliwa Sana na ukataji wa miti kwajili ya kuni na mkaa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati asilimia nane tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi na kwamba tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.


Kaim Mkurugezi wa Kampuni ya Taifa Gas Bhoke Angle akizungumza kwenye Uzinduzi wa kampeni ya Mazingira na matumizi ya Nishati safi na salama Mkoani Morogoro.


Share To:

Post A Comment: